2017-02-17 14:54:00

Maswali kwa Papa Francisko kutoka kwa wanafunzi Roma Tre


Chuo kikuu cha Roma Tre kilianzishwa kunako mwaka 1992. Hadi sasa kuna jumla ya wanafunzi 40, 000 waliosajiliwa. Ni chuo ambacho kina vitivo kumi na viwili na shule mbili. Ni chuo ambacho kinawaandaa wanafunzi kuingia katika soko la ajira kitaifa na kimataifa. Hapa ni mahali ambapo kiwango cha elimu kinadhibitiwa kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha kwamba ufundishaji wa maarifa na tafiti vinatekelezwa kadiri ya viwango vya kitaifa na kimataifa, ili kuwapatia motisha wafanyakazi na wanafunzi wanaosoma chuoni hapo! Chuo Kikuu cha Roma Tre ni kituo maalum cha tafiti za kimataifa na takwimu zinaonesha kwamba, ni kati ya vyuo vikuu bora vinavyoendelea kuibukia duniani!

Siku ya Ijumaa, tarehe 17 Februari 2017, Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Chuo Kikuu cha Roma Tre, alibahatika kuulizwa maswali na wanafunzi wanne. Nour Essa, mwenye umri wa miaka 31 kutoka Syria ameulizia kuhusu woga na wasi wasi unaooneshwa na raia wa Jumuiya ya Ulaya kwamba, wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria na Iraq wanahatarisha utamaduni wa Kikristo Barani Ulaya.

Niccolò Antongiulio Romano, mwenye umri wa miaka 23 kutoka Roma, ameomba kusikia ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mkristo aliyebahatika kukutana na Kristo Yesu katika maisha na leo yuko hivi alivyo sanjari na dhamana na utume wa Chuo kikuu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa upande wake Giulia Trifilio, mwenye umri wa miaka 25, kutoka Roma amemwomba Baba Mtakatifu Francisko kutoa dawa ya mchunguti itakayosaidia kupambana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia. Mwishoni, Riccardo Zucchetti mwenye Umri wa miaka 23 alibahatika kumuuliza Baba Mtakatifu swali kuhusu umuhimu wa utandawazi wa mshikamano utakaowawezesha wasomi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya upendo wa akili utakaosaidia kuipyaisha jamii?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.