Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Habari \ Habari za Kimataifa

Chuo Kikuu cha Roma Tre champongeza Papa Francisko kwa ushuhuda wake!

Chuo Kikuu cha Roma Tre kinampongeza Papa Francisko kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

17/02/2017 14:38

Professa Mario Panizza, Mkuu wa Chuo kikuu cha Roma Tre kilichoko mjini Roma, Ijumaa, tarehe 17 Februari 2017 amempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, ushuhuda wa maisha yake ni mwongozo makini kwa majiundo ya wanafunzi chuoni hapo. Chuo kikuu kinapania kuwa ni mahali pa kuleta mageuzi endelevu ndani ya  jamii kwa kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi na maarifa ya kuwa ni wasomi, wataalam na raia wa ulimwengu huu kwa “kufahamu kutenda” sanjari na “kufahamu kuwa”, kama kanuni maadili na majiundo makini katika maisha yao.

Chuo kikuu ni mahali pa kufundishia maarifa na kufanya tafiti, ili kuwawezesha wanafunzi kuzima kiu ya ufahamu na mageuzi, kwa lengo la kuishirikisha jamii katika mchakato wa ukuaji: kielimu, kimazingira na pamoja na huduma. Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi duniani ni matokeo ya kutokuwepo na uwiano wa maendeleo kati ya maeneo ya Kusini na Kaskazini; changamoto ya kusimama kidete kulinda na kudumisha amani chachu ya maendeleo endelevu. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinapaswa kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Professa Mario Panizza anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamekuwa ni chachu ya majadiliano ya kitamaduni ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kutajirishana kwa kushirikiana maendeleo ya kisayansi; kwa kuendeleza historia ya tamaduni mbali mbali. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni nafasi nyingine kwa Chuo Kikuu cha Roma Tre kuadhimisha kongamano kwa Mwaka 2017, sanjari na Kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Roma Tre, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya mji wa Roma, kwa kuzingatia tunu msingi za kiutu, tema za kijamii sanjari na maboresho ya kisayansi na kiteknolojia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

17/02/2017 14:38