2017-02-16 16:09:00

Upendo kwa jirani ndiyo bendera ya ukamilifu!


Mojawapo ya kanuni za kifalsafa ijulikanayo kama “Kanuni ya Dhahabu” inasema hivi: “usimtendee mwenzako lile ambalo hupendi kutendewa naye”. Mantiki ya kanuni hii yaweza kuelewaka katika upendo wetu kwa wenzetu. Kanuni hii inalenga kutupeleka katika kumtambua mwenzangu katika kipimo vya nafsi yangu. Yeye ni binadamu kama mimi, mwenye hisia, matamanio na hata wakati mwingine mapungufu kama ninayokuwanayo. Ni sawa na kusema kwamba njaa au kadhia ya namna yoyote inayopenya ndani ya nafsi yangu hupenya namna hiyo hiyo katika nafsi ya mwenzangu na hivyo vile ambavyo sipendi nitendewe na wengine nao kwa upande wao hawapendi kutendewa na katika kutendeana haki inatupasa kutokutendeana mabaya bali kupendana daima.

Uhalisia wa jamii inayotuzunga leo hii hutupatia changamoto nzito katika kuufikia ukamilifu. Visasi na uhasama ndilo jibu tunaloliona au tunalokusudia kwa yeyote ambaye amekutendea ubaya. Kristo anatupatia somo gumu na lenye changamoto ambalo ufahulu wake ndiyo kibali cha kutufikisha katika ukamilifu. Yeye anatutaka kuonesha upendo wetu kwa wote hata kwa anayekuhudhi. Yeye anayekunyima raha, anayekudhulumu, anayekupa mateso yawe ya kimwili au kisaikolojia apate jibu la upendo kutoka kwako. Sadaka yake ya kifo msalabani ni kielelezo kwetu kwani katika hali ya mateso vile anafikiria wema kwa wale wanasababisha mateso hayo: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”. Lk. 23:34.

Sala ya Kristo Msalabani ya kuwaombea watesi wake inatufumbulia jambo la muhimu ambalo tunapaswa kulijenga daima ndani ya nafsi zetu. Kristo anawaona kuwa hawana ufahamu wa walitendalo kwa mwanadamu mwenzao. Badala ya kuonesha upendo na huruma wanafanya ukatili kwa ajili ya kuupindisha ukweli. Tunaalikwa kutambua kwamba yeyote anapoonekana kututendea uovu anapaswa kuonekana kuwa anatenda katika hali ya giza, katika hali ya kutokutambua yeye ni nani. Hivyo hatupaswi kulumbana naye wala kumjibu kwa kisasi bali ni kutafuta namna ya kumrudisha katika mstari. Huyu anakuwa amepungukiwa na ufahamu wa hadhi yake na hivyo hatendi kwa ufahamu.

Mwanadamu ameumbwa akiwa katika hali ya ukamilifu. Ukamilifu wake huu unaonekana katika nyanja zote zikiwa pamoja na mahusiano kati ya mtu na mtu. Mwenyezi Mungu katika hekima yake amemjenga mtu kuwa na uhusiano wa kirafiki na mwenzake; amemjenga mtu awe na nia njema kwa ajili wa wengine. Mambo ambayo yanajenga uadui kati yetu ni uthibitisho wa kupindishwa kwa hali hiyo. Tangu dhambi iingie ulimwenguni tumebaki katika hali ya kudhaniana vibaya, kutokupendana na hata kunia mabaya kwa ajili wa wengine. Mafanikio ya mwenzangu si furaha kwangu bali ni karaha. Mateso ya wengine na kushindwa ndiyo nia ya moyo wangu. Hali hii inanifanya kupoteza ukamilifu.

Kipimo cha ukamilifu wetu ni Mungu. Ingawa sisi tunaendelea kumfanyia uhasi anaendelea kutuonesha upendo wake. Hii ni kwa sababu kinachomchukiza Mungu ni dhambi lakini zi hadhi yake yeye anayetambulika kama mdhambi. Mwenyezi Mungu anajua katika hekima yake kwamba kinachomwaribu au kumpatia sifa mbaya mtu si hadhi yake, si sehemu ya asili yake bali ni uvamizi wa matamanio ya adui mwovu ambaye daima anatafuta namna ya kumwangusha mwanadamu na kujiongezea wafuasi. Leo hii anatualika kwa kusema: “kuweni watakatifu kama mimi nilivyo mtakatifu”. Mungu pia huwamiminia baraka zake watu wote kwa maana “huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”. Yeye anatufunulia utakatifu wake huo kwa njia ya Kristo anayetualika leo kupiga hatua moja zaidi ya watu wa ulimwengu huu.

Upendo wetu kwa jirani unatutafakarisha juu ya neno hilo jirani. Jirani yangu huyu ni nani? Je, ni yule anayenitendea mema tu? Je, ni yule aliye upande wangu? Changamoto ya Kristo ni hii: “mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mtapata thawabu gani?, hata watoza ushuru; je! hawafanyi yayo hayo?” Upendo wa Kristo ni ule unaomwalika kila mmoja kutoka na kuitafuta nafsi yake katika nafsi ya jirani yake. Ni ule upendo ambao unatafuta ustawi na fanaka ya wengine kusudi kwa ukamilifu wao kuweza kuleta amani kati ya mtu na mtu au jamii na jamii. Kupenda mtu anayekupenda ni sawa na kulipia kile ambacho amekutendea. Mkristo anapaswa kutenda cha ziada kwa wengine; mkristo anapaswa kujisikia mdeni wa matendo mema kwa wengine.

Hali halisi ya jamii ya mwanadamu leo hii inatuita kuufanyia kazi wito huu. Amani imetoweka kuanzia ngazi za familia hadi taifa kwa ujumla na kwenda hata katika ngazi ya kimataifa. Masuluhisho mengi yanayotafutwa si kwa ajili ya kuustawisha upendo kwa jirani bali ni kutaka kumwangamiza na matokeo yake ni kuzidisha uhasama. Miito mbalimbali ya kinabii ya kufanya mazungumzano hugeuziwa kisogo na kuendelea kumwangamiza mwanadamu mwili na roho. Dunia imebaki katika falsafa ya jicho kwa jicho au jino kwa jino. Bila kutoka katika muono huo wa kulipizana visasi na kuwekeana vinyongo hatuwezi kupata amani katika familia zetu, hatuwezi kuwa na uelewano katika jamii yetu na hatuwezi kuijenga amani kati ya taifa na taifa.

Mtume Paulo anatualika kuitambua hadhi tuliyonayo ndani mwetu, yaani kuwa tu hekalu la Mungu. Wajibu wetu ni kumpatia nafasi Roho Mtakatifu aliye ndani mwetu atende kazi na hivyo kutenda si kwa hekima za kidunia bali kwa hekima ya Mungu. Hekima hiyo inafunuliwa kwa njia ya Kristo ambaye ni kielelezo kwetu kwa mapendo ya jirani. Tunapojitahidi kufikiri katika akili zetu bila kuitanguliza hekima yake tunajikuka tumejifunga katika utitiri wa masuluhisho ambayo badala ya kutujenga huishia katika kutugamwanya na kutotoa nafasi kupata amani. Hii ni kwa sababu kila mmoja atatafuta huria ya maadili kadiri aonavyo yeye na katika huria hiyo wote watakuwa wanatafuta haki ya kusikilizwa na kutahminiwa mawazo yao.

Tujivike muono wa Mungu katika ukamilifu wake. Tuwapokee wanaotuudhi na kututendea mabaya kama wale ambao wamepungukiwa ufahamu, hawalifahamu walitendalo na hivyo wanahitaji kusaidiwa. Ingawa waswahili wanasema dawa na moto ni moto lakini kikristo dawa yake ni kuuzima na pia ingawa tunaambiwa adui mwombee njaa au tunamtakia kushindwa sisi tusibaki huko bali tuwaombee heri ili neema za Mungu zipate nafasi nafsini mwao na hivyo kuwakomboa katika hali ya uovu waliyo nayo. Na hivyo “mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.