2017-02-16 15:03:00

Damu ya watu wasiokuwa na hatia inawalilieni!


Vita inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu, kumbe kila mtu anapaswa kujizatiti kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Watu wengi sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kutokana na baadhi ya watu wanaoelemewa na uchu wa: fedha, mali na madaraka; watu wanaotaka kuchuma faida kubwa kwa njia ya biashara haramu ya silaha inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 16 Februari 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amekita mahubiri yake katika alama kuu tatu yaani: Njiwa, Upinde wa mvua na Agano na Nuhu; mambo msingi yaliyojitokeza kwenye Somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Mwanzo; alama ambazo kimsingi ni dhaifu sana, lakini Mwenyezi Mungu anazitumia kwa ajili ya kufunga Agano la Nuhu, ili kulinda na kudumisha amani, ingawa si rahisi sana kwa mwanadamu kudumisha amani moyoni mwake. Mwenyezi Mungu anamkanya Nuhu na jamaa yake kutomwaga damu ya mwanadamu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Pale mwanadamu anapomwaga damu ya jirani yake, atambue kwamba anatenda dhambi na atawajibika mbele ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii dunia imegeuka kuwa ni uwanja wa vita, watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kumwaga damu kutokana na uchu wa fedha, mali na utajiri wa haraka haraka; hawa ni watu wanaotaka kukwapua maeneo makubwa ya ardhi kutoka kwa wanyonge; wanataka kupata faida kubwa kwa biashara haramu ya silaha; lakini wote hawa wanapaswa kukumbuka kwamba, wanawajibika mbele ya Mungu kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Waamini wanaodhani kwamba, wana amani na utulivu, wanapaswa kuwajibika kuwatetea wale wote wanaojikuta wametumbukizwa katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kwani amani ni dhamana ya wote. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, vita kimsingi inapata chimbuko lake kutoka katika moyo wa mwanadamu na hatimaye, inaanza kusambaa katika familia, jamii ya watu na hatimaye, kuenea sehemu mbali mbali za dunia. Chanzo cha vita ni wivu usiokuwa na mashiko; ni matokeo ya kiburi cha mwanadamu. Kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani kati ya watu kwani hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu kwa kumwaga damu yake azizi pale Msalabani ameupatanisha ulimwengu na Mwenyezi Mungu. Vita inapohitimishwa, watu wanapata amani na utulivu wa moyo; vita hii inapaswa kusitishwa kwanza kabisa katika sakafu ya mioyo ya watu, katika familia, jamii na sehemu mbali mbali za dunia anasema Baba Mtakatifu. Kwa njia hii, njiwa, upinde wa mvua na agano kati ya Mungu ingawa ni dhaifu, vitaweza kuimarishwa kwa msaada na neema ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.