2017-02-15 15:55:00

Wanandoa watarajiwa wanahitaji majiundo makini!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, kuna haja ya kuwa na Ukatekumeni mpya katika maandalizi ya maisha ya ndoa na familia, ili kweli vijana wa kizazi kipya waweze kutambua na hatimaye kuwa ni mashuhuda na vyombo vinavyotangaza; utakatifu, ukuu na wema unaofumbatwa katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko katika wosia wake wa kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” anawaalika wanandoa kuwa kweli mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika furaha.

Kardinali Baldisseri ameyasema haya huko Terni, Italia kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Wapendanao, maarufu kama “Valentine Day”. Wanandoa watarajiwa wanakumbushwa kumkimbilia Mtakatifu Valentino, ili kumwomba ulinzi na tunza yake katika safari ya maandalizi ya maisha ya Ndoa na familia. Tarehe 14 Februari 2017 imekuwa pia ni fursa ya kukazia umuhimu wa majiundo awali na endelevu kwa wanandoa watarajiwa, ili kweli familia iweze kuwa ni kisima cha furaha na unyenyekevu; kwa kutambua udhaifu na mapungufu yao kama binadamu; daima wakijiaminisha kwa huruma na neema ya Mungu katika safari ya maisha yao ya ndoa na familia.

Kardinali Baldisseri amewataka wanandoa watarajiwa kujiandaa vyema kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa Takatifu ambayo kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya wanandoa wenyewe, kwa ajili ya kuzaa watoto ambao daima ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuwapatia malezi bora na makini, ili kweli watoto hawa waweze kuwa Wakristo watakatifu na raia wema. Dhamana ya malezi na majiundo awali na endelevu inapaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kusaidiana na waamini walei waliobobea katika maisha na utume wa ndoa na familia, ili kubadilishana uzoefu na mang’amuzi katika maisha ya ndoa na familia; uzuri, matatizo na changamoto zake, ili hatimaye, wanandoa wenyewe waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia.

Wanandoa watarajiwa wanapaswa kupata majiundo makini kuhusu dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Ndoa na familia, ili kupanga na kuratibu masuala ya kazi na ajira; elimu na malezi kwa watoto wao; mahusiano na mafungamano kwa wazazi, ndugu na jamaa. Wanandoa watarajiwa, wanapaswa kujiridhisha kabisa kwamba, mambo msingi katika maisha yao wameyaweka hadharani pasi na wasi wasi, lakini pale ambapo bado kuna kivuli cha wasi wasi, mashaka na woga ni afadhali kupeana muda ili kuondoa mashaka na wasi wasi hizi, kwani mara nyingi mambo haya ndiyo yanaweza kuibuka na kuwa ni chanzo cha vurugu, kinzani na mipasuko ndani ya familia.

Kardinali Baldisseri anakaza kusema, Mihimili ya Uinjilishaji yaani: Wakleri, Watawa na Makatekista wanapaswa kuwa wamefundwa barabara ili kuwasaidia wanandoa watarajiwa katika majiundo ya maisha ya ndoa na familia. Wanandoa watarajiwa wafahamishwe wapi wanaweza kupata msaada wa haraka wanapokabiliwa na dharura, magumu pamoja na changamoto ya maisha za ndoa na familia. Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na majiundo awali na endelevu katika maisha ya ndoa na familia, kama inavyokuwa pia kwa Wakristo kuendelea kufundwa katika maisha yao kwa njia ya Ukatekumeni mpya.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kwa wana ndoa watarajiwa, sanjari na kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wa familia, ili kuweza kukabiliana na changamoto za miaka ya awali ya maisha ya ndoa na familia, kwa mfano wanapopata mtoto wao wa kwanza. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko kuchapisha Wosia wake wa Kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” ni kuonesha jinsi ambavyo Kanisa linaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya ndoa na familia. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia na Sinodi ya Maaskofu kwa vijana itakayoadhimishwa mwaka 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Mkazo ni wanandoa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha, mang’amuzi pamoja na kuwasindikiza waamini katika maisha na utume wa ndoa na familia anasema Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.