2017-02-15 15:24:00

Matumaini ya Kikristo hayadanganyi yamejikita katika upendo wa Mungu


Matumaini ni zawadi ya ajabu sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu; waamini wanaalikwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa jirani zao, ili kama watoto wa Mungu, wajifunze kuwafariji na kuwategemeza jirani zao katika huruma ya Mungu ambayo kamwe haiwezi kumtenga mtu awaye yote. Matumaini ya Kikristo hayawezi kamwe kumdanganya mtu kwani yanafumbatwa katika upendo wa Mungu unaoyarutubisha kwa kila mwamini. Mtakatifu Paulo anakaza kusema kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Waamini wanakumbushwa kwamba, wamehesabiwa, wamepatanishwa na kuokolewa na Mwenyezi Mungu.

Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 15 Februari 2017 kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi yake kuhusu matumaini ya Kikristo na kwamba, “Kamwe matumaini hayawezi kumdanga mtu”. Hakuna sababu ya kujisifia na kujigamba, kwani Waswahili husema, eti debe tupu haliachi kutika! Kwa kujigamba sana kunaweza kuwakosea watu wengine haki zao, hasa wale ambao hawajabahatika sana, hiki ni kielelezo cha kiburi cha binadamu.

Mtakatifu Paulo anapowaandikia Warumi anawataka kujisifia kwa sababu wamehesabiwa haki itokayo katika imani, kumbe wanapaswa kuwa na amani kwa Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo ambaye amewawezesha yote haya kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo wanasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Hii ni zawadi inayopaswa kumwilishwa ili kutenda kazi katika historia na katika maisha ya watu, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao.

Upendo ni zawadi na kielelezo cha mpango wa Mungu katika historia ya wokovu inayopata utimilifu wake kwa njia ya Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo. Waamini wanahamasishwa kutambaua na kuipokea zawadi hii kwa moyo wa shukrani na hivyo kuwa ni chemchemi ya sifa, baraka na sifa kuu. Kwa kutekeleza haya wanakuwa na amani kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anayewashirikisha mang’amuzi ya uhuru kamili. Amani ambayo waamini wanakirimiwa na Mwenyezi Mungu inapaswa kuenea katika medani mbali mbali za maisha na mahusiano ya watu; katika maisha yao binafsi, ndani ya familia, jumuiya, maeneo ya kazi na kwa watu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Mtakatifu Paulo anawataka waamini kufurahi katika dhiki kwa kutambua kuwa dhiki kazi yake ni kuleta saburi na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo na kazi ya uthabiti wa moyo ni matumaini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwelekeo huu si  rahisi sana katika maisha ya waamini, kwani shida na mahangaiko ni sehemu ya chakula chao cha kila siku. Amani inapata chimbuko lake katika imani ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kielelezo cha neema na upendo wa Mungu ambaye daima anatembea pamoja na waja wake katika maisha yao, hali ambayo inasaidia kuleta saburi kwa kutambua kwamba, hata katika nyakati za giza na wasi wasi mkubwa huruma na wema wa Mungu bado ni mkubwa kupita yote na hakuna kitu chchote kinachoweza kuwapokonya kutoka katika umoja na uwepo wa Mungu katika maisha yao.

Kutokana na ukweli huu, matumaini ya Kikristo ni thabiti na kamwe hayadanganyi kwani yanafumbatwa katika upendo wa Mungu anayeyarutubisha kila kukicha! Baba Mtakatifu anasema, ni rahisi sana kusema, Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake, lakini wengi wana mashaka kama kweli Mungu anawapenda. Waamini watambue kwamba, upendo wa Mungu umekwisha kumiminwa katika mioyo yao na Roho Mtakatifu waliyempokea. Upendo wa Mungu ni kiini cha usalama na matumaini ya waamini, ambayo yanageuzwa kuwa ni sala.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini waone fahari juuu ya upendo wa Mungu kwao na hakuna kitu kinachoweza kuwatenga na upendo huo, changamoto kwa waamini ni kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini katika unyenyekevu na kiasi kwa ajili ya wote, kwani Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote, anayewapenda na kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi. Jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kujifunza kufarijiana na kuinuana, kwani matumaini ya Kikristo kamwe hayamdanganyi mtu! Ujumbe huu usaidie kuhamasisha ushuhuda wa Kikristo katika familia na jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.