2017-02-13 10:49:00

Wanaojihusisha na dawa za kulevya Tanzania sasa kuchezeshwa vidogori!


Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imeamua kupambana kufa na kupona na janga la biashara haramu za dawa za kulevya kwa kuzingatia: kanuni, sheria na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuwasaidia waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuwachukulia hatua kali watengenezaji, wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya ambazo ni hatari kwa usalama, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Tanzania.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, anaitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, badala ya mwelekeo wa sasa unaofanywa na baadhi ya watanzania kukejeli hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya janga hili la kitaifa ambalo limeleta majanga makubwa kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa. Kardinali Pengo kwa macho makavu kabisa anasema, hata Wakristo wamo katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kumbe, kuna haja ya kushirikiana na Serikali ili kuunda mazingira yatakayoimarisha afya ya jamii miongoni mwa watanzania.

Wakristo na viongozi wa Kanisa watambue wajibu na dhamana yao katika kulinda, kudumisha afya ya binadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa Katoliki liwe mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa kukazia malezi, kanuni maadili, utu wema, mafao ya wengi na kiasi ili kuondokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka kwa njia za mkato na baadhi ya vijana kudhani kwamba, kilele cha mafanikio yao ni kubwia dawa za kulevya. Vijana waelimishwe kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, mafanikio yanakuja kwa juhudi, maarifa, nidhamu na kujituma, kumbe wanapaswa kufanya maamuzi sahihi na thabiti katika maisha.

Kwa bahati ambaya anasikitika kusema Kardinali Polycarp Pengo kwamba, wafanyabiashara wa dawa za kulevya pengine hata wao wenyewe hawazitumii, lakini wanawatumia vijana maskini kutokana na umaskini wao kuendelea kuwatumbukiza wengine katika baa la umaskini wa hali na kipato kwa njia ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na hivyo kuwa ni mzigo mkubwa kwa familia na taifa katika ujumla wake! Umefika wakati kwa watanzania kuunga mkono mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya anasema Kardinali Pengo katika mahojiano maalum na Gazeti la Kiongozi linalomilikiwa na kuchapishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Kwa upande wake, Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara anasema, wakati Tanzania inapambana na janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kuna haja kwa jamii, serikali na viongozi wa kidini kutafakari kwa kina sababu msingi zinazowatumbukiza baadhi ya watu katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kweli mapambano haya yaweze kuganga na kuponya chanzo cha janga hili kitaifa. Hapa kuna haja ya kusimama kidete kukata mzizi wa fitina unaosababisha watu kutaka kujitumbukiza katika uuzaji, usambazi na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Ikiwa kama watanzania watafanikiwa kuganga na kuponya chanzo cha biashara haramu ya dawa za kulevya, itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya inayoendelea kutishia usalama, utu, heshima na mafungamano ya kijamii, kwani hii ni vita ambayo tayari imewagusa na kuwatikisha viongozi wa kidini na kisiasa; wafanyabiashara maarufu; wasanii na watu wa kawaida ambao pengine wanatumiwa tu na “vigogo” wa biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo imepelekea watanzania kadhaa kufungwa ndani na nje ya nchi kwa kujihusisha na biashara, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya kutaja hadharani majina ya watuhumiwa na kutakiwa kufika kituo kikuu cha Polisi Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na Jeshi la Polisi. Moto huu mkali umewashwa na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ambaye ameamua kujitosa kimasomaso ili kuwajibika kuwanusuru watanzania wanaotumbukizwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwani anajisikia kuwajibika kimaadili mbele ya Mwenyezi Mungu.

Rais John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba vinaongeza nguvu katika mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kusimamia sheria na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka. Katika vita hii, Dr. Magufuli amedhamiria kweli kweli kwani tayari amekwisha mteua na kumwapisha Kamishina mkuu wa Mamlaka ya kuzia na kupambana na dawa za kulevya Roger Sianga; Kamishina wa Operesheni Bwana Mihayo Msikela pamoja na Kamishna wa Intelijensia Bwana Fredrick Kibuta, Kikosi maalum kinachoonesha dhamiri ya Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kwa namna ya pekee, viongozi wa kidini wanakazia umuhimu wa kuzingatia haki msingi za binadamu, utu na heshima yao pamoja na haki ya mtuhumiwa, ili kweli mapambano haya yaendeshwe katika misingi ya sheria kwa kuzingatia haki!

Habari zaidi kutoka Ikulu zinasema kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha vinasimamia sheria ipasavyo ili kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini. Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers William Siyanga, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Joseph Edward Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Omar Yusuf Mzee na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Grace Aaron Mgovano. Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wa Serikali kuungana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na ametaka mapambano hayo yasifanywe kwa mzaha wala kwa kuangalia majina ya watu, vyeo vyao na taasisi wanazoongoza.

Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na amewaomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya biashara na kutumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya Taifa. “Niwaombe ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya, waandishi wa habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania wetu, akitokea mtu anapambana na dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya kumchafua. “Vita hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na Serikali itahakikisha inasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Anna Makinda na sheria hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria hii.” Amesisitiza  Rais Magufuli.

Pia, Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha kuna watanzania 1,007 wamekamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, na amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kutojihusisha kuwatetea waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake waache sheria za nchi husika zichukue mkondo wake.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemtaka Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Idara ya Uhamiaji nchini kutokana na utendaji wake kutoridhisha. “Nataka ukafanye mabadiliko makubwa (Total Reform), nataka Uhamiaji izalishe fedha kwa ajili ya nchi hii, nataka ukadhibiti utoaji hati za kusafiria (Passports) maana zimekuwa zikitolewa hovyo hovyo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli. Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao pamoja na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Na Sara Pelaji kutoka Gazeti la Kiongozi & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S na Ikulu, Tanzania.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.