2017-02-13 08:46:00

Sikilizeni kilio cha wakimbizi na wahamiaji!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kaskazini,  CERNA, limehitimisha mkutano wake ulioadhimishwa huko Senegal. Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi kutoka Barani Afrika kuelekea Ulaya pamoja na changamoto zake pamoja na majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, ni mada zilizopembuliwa wakati wa mkutano huu. Askofu mkuu Paul Jacques Marie Desfarges S.J, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Algiers ndiye aliyeongoza mkutano huu.

Kardinali Thèodore Adrien Sarr, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dakar, aaliwaongoza Maaskofu wenzake katika mafungo ya maisha ya kiroho na baadaye Maaskofu hawa wakapata nafasi ya kutembelea Majimbo mbali mbali nchini Senegal ili kukutana na familia ya Mungu. Maaskofu hawa pia walikutana na kuzungumza na Rais Macky Sall wa Senegal. Wamempongeza pia Askofu George Bugeja aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa niAskofu mpya wa Jimbo la Kitume la Tripoli, Libya baada ya Askofu Giovanni Martinelli kung’atuka kutoka madarakani hivi karibuni.

Maaskofu katika mkutano wao wamekazia umuhimu wa waamini kuonesha mshikamano wa upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Hiki ni kipaumbele cha pekee kwa familia ya Mungu Kaskazini mwa Afrika ambako kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta fursa ya kwenda Barani Ulaya. Injili ya upendo na ukarimu iwe ni dira na mwongozo kwa ajili ya kuwasaidia na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji Kaskazini mwa Afrika.

Maaskofu wanakaza kusema, wakimbizi na wahamiaji wanahitaji kusikilizwa kwa makini, kwani hawa ni watu walioguswa na kutikishwa utu na heshima yao kama binadamu kutokana na changamoto zinazowaandama. Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki katika Majimbo na Parokia, yameendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, licha ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo. Kumekuwepo pia ushirikiano wa kiekumene na kidini katika kuwahudumia wakim bizi na wahamiaji huko Afrika ya Kaskazini. Maaskofu wanakiri kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa katika karne ya ishirini na moja. Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, Jumuiya za Kikristo zitaendelea kuchangia kwa hali na mali katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na Serikali husika kuhakikisha kwamba, zinatafuta majibu muafaka ili kuweza kukabiliana na changamoto na fursa ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Kaskazini mwa Afrika.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika linakiri kwamba, linakabiliwa na uhaba wa mihimili ya Uinjilishaji yaani: Wakleri na Watawa ambao wangeweza kusaidia kutoa huduma kwa wanafunzi; wakimbizi na wahamiaji kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kushirikiana na Jumuiya za Kikristo katika Makanisa mahalia. Maaskofu wanawaalika Wakristo kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Mafungamano ya kijamii na waamini wa dini ya Kiislam wanasema Maaskofu ni utajiri mkubwa kwa familia ya Mungu Barani Afrika katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wakristo na Waislam wanaweza kuishi kwa amani na utulivu bila migogoro wala kinzani, mambo ambayo wakati mwingine yanatumiwa na baadhi ya watu kuvuruga umoja  na mshikamano kwa mafao yao binafsi.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, bado kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu Afrika ya Kaskazini kujizatiti zaidi na zaidi katika kukabiliana na matatizo yao, tayari kuyapatia ufumbuzi wa kudumu, ili kweli amani na utulivu visaidie kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Ubora wa maisha ya Kikristo haufumbatwi kwa idadi ya waamini wanaohudhuria ibada Kanisani, bali katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kuyachachua malimwengu kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili. Kumbe, Wakristo wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika litakutana tena kuanzia tarehe 19- 22 Novemba 2017 huko Tunis, Tunisia kwa mkutano wao wa pili wa mwaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.