2017-02-13 07:46:00

Makanisa na mapambano dhidi ya utumwa mamboleo duniani!


Viongozi wakuu wa Makanisa wanalaani kwa nguvu zote mifumo mipya ya utumwa mamboleo unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanasikitika kusema, biashara ya utumwa hata katika nyakati zilizopita ilikuwa ni kero, ukiukwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu na usumbufu kwa watu waliokuwa wanatekwa nyara na kutumbukizwa katika biashara hii haramu! Haya ni maneno mazito yaliyomo kwenye tamko lililotiwa sahihi na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli pamoja na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani, baada ya kukutana kwa pamoja kati ya wajumbe wa Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Anglikani kuanzia tarehe 5- 6 Februari 2017 huko Istanbul, nchini Uturuki.

Kwa muda wa siku mbili, wajumbe hawa wamefanya kongamano la kidini lililojadili kwa kina na mapana madhara ya utumwa mamboleo, kwa kuwashirikisha mabingwa, wataalam na viongozi wa Makanisa ambao daima wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na biashara haramu ya binadamu, ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza ambaye ameutangaza Mwaka 2017 ni kuwa ni “Mwaka wa kulinda utakatifu wa watoto” sanjari na kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi; mambo yanayofumbatwa katika uhuru wa binadamu.

Wajumbe wamekumbushwa maamuzi yaliyotolewa kwenye Mtaguso wa Makanisa ya Kiorthodox uliofanyika mjini Creta, huko nchini Ugiriki ambako viongozi wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox walikaza kusema, Kanisa lipo na linaishi kwa ajili pamoja na watu na wala si kwa mambo yake binafsi. Viongozi wa Makanisa haya mawili wamekubaliana kimsingi kuunda Kikosi kazi kitakachosimama kidete kupambana na mifumo wa utumwa mamboleo sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza amesikitika kusema kwamba, Kanisa la Kiorthodox mara nyingi linashutumiwa kwa kujikita zaidi katika Ibada, Liturujia na Maisha ya kiroho zaidi, lakini kwa kongamano hili, Kanisa linataka kuwaonesha walimwengu kwamba, liko kwa ajili ya ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu! Kanisa linataka kusimama kidete kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaoendelea kutumbukizwa katika lindi la utumwa mamboleo. Imani ya kweli haina budi kusimama kidete kupambana na Shetani, baba wa maovu yote duniani.

Kwa upande wake Askofu mkuu Justin Welby amesikika akisema, Kanisa linataka kujizatiti kupambana kufa na kuponya dhidi ya mifumo yote inayomnyanyasa na kumdhalilisha mwanadamu; kwa kuwatumbukiza watu katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utalii wa ngono na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo, wanawake na wasichana. Haya ni mambo yanayofanyika katika barabara na mitaa kadhaa duniani, lakini watu wanayafumbia macho kana kwamba, hakuna kitu kinachotendeka! Umefika wakati wa kufungua macho na masikio ili kuona na kusikiliza kilio cha maskini na watu wanaodhalilishwa kutokana na mifumo ya utumwa mamboleo. Viongozi wa Makanisa wanasema, kuna haja pia ya kusimama kidete kulinda na kudumisha sera za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya kazi ya uumbaji na mazingira. Utumwa mamboleo ni matokeo ya uchu wa fedha na mali; kiburi na majivuno ya binadamu; mambo yanayowadhalilisha watu wengine kwa ajili ya kukinufaisha kikundi cha watu wachache katika jamii, jambo ambalo si haki kabisa!

Viongozi wa Makanisa katika tamko lao la pamoja wanakaza kusema, utumwa mamboleo ni janga kubwa linaloendelea kumwandama mwanadamu katika karne ya ishirini na moja, kiasi cha kutishia maisha, usalama na mafungamano ya kijamii. Hii ni dhambi kubwa inayotikisa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Viongozi wa Makanisa wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na utumwa mamboleo. Watu waone na kuonja mateso ya waathirika wa utumwa mamboleo ili waweze kufikiri na kutenda kwa haki. Watu watahukumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kile ambacho wanashindwa kutenda kwa kuongozwa na dhamiri nyofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.