2017-02-13 07:08:00

Majadiliano ya kidini ni muhimu katika ujenzi wa amani na maendeleo!


Majadiliano ya kidini yanapaswa kuwa ni mpango mkakati unaomwilishwa katika ngazi mbali mbali za maisha ya waamini, kuanzia kwenye familia, masuala ya kidiplomasia pamoja na mwingiliano wa tamaduni kati ya watu, ili kujenga msingi wa maridhiano, umoja na udugu, kwa kutambua kwamba, tofauti za kidini si chanzo cha kinzani, bali ni utajiri unaopaswa kufumbatwa na wote, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Urafiki na udugu ni mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia katika maisha na utume wa Kanisa.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye Makao yake Makuu mjini Geneva, Uswiss. Majadiliano ya kidini katika urafiki na udugu yanalenga kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii kati ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili kushirikiana na kushikamana, tayari kuwajibika kwa ajili ya ustawi wa wengi. Mahusiano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali yanapaswa kusimikwa katika udugu unaowajibisha badala ya kuendelea kukazia dhana ya maridhiano kati ya watu, kwani udugu unawatajirisha waamini wote kwa kufumbata na kuambata tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu ili kuendelea kuboresha mahusiano yake na jirani zake, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Mashambulizi ya kigaidi, utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia ni tishio kubwa kwa amani duniani.

Chanzo kikuu cha vita, kinzani na mipasuko ya aina mbali mbali duniani anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovic, ni matokeo ya mwono finyu kuhusu mwanadamu na haki zake msingi; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, hapa kuna haja kwa waamini kujikita katika majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, ili kutambua utu na heshima ya binadamu; haki zake msingi, ili kwa pamoja kuibua mbinu mkakati wa kulinda na kudumisha mazingira bora, nyumba ya wote. Katika mchakato huu, viongozi wa kidini wanayo dhamana nyeti na pevu inayojikita katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, usawa na mafao ya wengi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, haki na amani ni mambo ambayo yamefichika katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ni kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha utamaduni wa amani na madaraja ya watu kukutana, kushirikiana na kusaidiana kwa dhati! Udugu na mshikamano vinapaswa kukuzwa na wote, ili kuamsha ndani mwao ile kiu na hamu ya mafao ya wengi; tayari kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho kati ya watu, hususan kwenye maeneo ambayo yamegeuka kuwa uwanja wa fujo na mauaji ya kutisha.

Kwa bahati mbaya anakaza kusema, Askofu mkuu Ivan Jurkovic kwamba, kuna baadhi ya wanasiaasa wachache wanaopenda kutumia udini na ukabila kuwa ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwa ajili ya faida zao binafsi, yaani uchu wa mali na madaraka! Dini zinapaswa kuwa ni kiungo maalum cha upendo, mshikamano na udugu kati ya watu na kamwe kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, yanaweza kusaidia kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho kama ilivyojitokeza katika Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, leo hii familia ya Mungu nchini humo inaendelea kuandika ukurasa wa historia mpya ya nchi yao kwa kukataa kugawanywa kwa misingi ya udini na ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wengi!

Majadiliano ya kidini na kiekumene ni dhana inayowezekana kabisa kama ilivyoshuhudiwa kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Cyrill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima walipokutana wakasali na kuzungumza huko Cuba! Askofu mkuu Ivan Jurkovic anahitimisha hotuba yake kwa kusema haki, amani, msamaha na upatanisho ni chanda na pete kwani ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana; ili kujenga umoja, udugu na mshikamano wa kweli. Hakuna amani ya kweli pasi na haki na wala hakuna haki ya kweli pasi na msamaha! Kumbe basi, waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.