Katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu, Francisko; "Misericordia et misera" yaani: Huruma na amani, tunakutana na ujumbe muhimu sana katika maisha ya mkristo, na ujumbe huo si mwingine bali ni adhimisho la Sakramenti ya Upatanisho au kwa maneno mengine Sakramenti ya Kitubio. Katika adhimisho la sakramenti hii ya upatanisho kila mkristo anapata kushishiriki kwa kina adhimisho la Huruma ya Mungu, ambapo huruma hii hutuletea msamaha na faraja, na hivyo kupata amani na utulivu moyoni. Hivyo kwa Huruma hii ya Kimungu, tuipatayo kupitia sakramenti ya upatanisho yatuunganisha tena na Mungu na kumfanya mkristo kujisikia upya tena rohoni, jambo ambalo linamfanya Mkristo, kujisikia kukutana tena na Mungu. Mungu ajae kutujalia neema ya kuwa tena watoto wake.
Katika hali yetu ya kibinadamu twatambua ya kuwa sisi ni wadhambi na maranyingi tunamkosea mwenyezi Mungu, lakini daima Mungu anatujia katika uso wa huruma na kutupa upatanisho na msamaha. Katika hili Mungu anatufanya tutambue ujumbe wake na hasa katika kutaka kuwaokoa wanyonge na wadhambi. Hivyo Mtakatifu Paulo anatuambia neema ina nguvu kuliko dhambi, na hii neema hutufanya tuyapite mapito yote, hata yawe magumu namna gani, kwa sababu katika upendo wa Mungu twayapita yote. Katika Sakramenti ya Upatanisho, Mungu anatuonyesha njia ya kurudi kwake, na hivyo kutukaribisha na kutufanya wapya katika yeye, na unakuwa ni mwanzo tena wa kuishi katika upendo na katika umoja na Mungu. Mtakatifu Petro anatuasa haya anapotuambia, upendo husamehe dhambi na Mungu tu aweza kusamehe dhambi ila pia Mungu anatualika kupata kusameana wenyewe kwa wenyewe, kuwasamehe pia hata walio tukosea na kutujeruhi.
Baba Mtakatifu anatualika kutafakari tena maneno ya Mtakatifu Paulo, hasa pale alipokiri kwa Timotheo ya kwamba, yeye alikuwa mdhambi mkubwa na kwa sababu hiyo alipokea neema, ya wongofu. Maneno haya yatufanya tutafakari upya maisha yetu na kuona huruma ya Mungu ikituletea mabadiliko na wongofu wa ndani. Kwa tafakari zaidi Mtakatifu Paulo anaendelea kutuambia Mungu ametupatanisha sisi na yeye kupitia mwanae Bwana Wetu Yesu Kristo, ambaye katika yeye twapokea ujumbe wa upatanisho, na tunafanywa mashahidi wa huruma na Msamaha wa Mungu.
Katika Sakramenti ya Upatanisho, Mkristo anaitwa kuishi tena upya wa Injili, kuishi tena kiundani fadhila za Kiinjili, na zaidi kupata kuamini nguvu itokanayo na neema ya Kimungu, na kwa namna hii twakaribia zaidi na zaidi ule upendo wa Mungu baba ambao watupa nafasi kubwa ya ile nguvu ya msamaha. Kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kila Mkristo anaonja tena upendo wa Mungu Baba, kwa kupatanishwa na Mungu na kufanywa wapya katika Kristo. Hivyo basi, kwa unyenyekevu na moyo na toba tukumbuke kumwendea Mungu na kupokea Sakramenti ya upatanisho kupitia wajumbe wake aliowateua na kuwapa neema ya kuadhimisha Sakramenti hii yaani makuhani. Matokeo ya Sakramenti ya Upatanisho ni amani na furaha moyoni, na hii ni ile furaha ya kuunganika tena na Mungu na kuukumbatia upendo wa Mungu, upendo usiokuwa na kikomo. Hivyo kwa mwaliko huu wa Furaha na amani tujongee wote katika Huruma ya Mungu Baba kupitia Sakramenti ya Upatanisho.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Agapiti Amani, ALCP/OSS.
All the contents on this site are copyrighted ©. |