2017-02-11 10:16:00

Papa Francisko "kutinga timu" Chuo kikuu cha Roma Tre"


Hati ya Maandalizi kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” inaonesha jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyowathamini vijana katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Anawataka vijana kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Kanisa linataka kuwasikiliza vijana kwa makini, kuona ushuhuda wa imani yao katika uhalisia wa maisha; wasi wasi na madongo wanayotaka kulitupia Kanisa kuhusiana na utume wa Kanisa kwa vijana. 

Baba Mtakatifu Francisko kwa muda wa miaka mitatu anawataka vijana kumjifunza Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria: kwa kusikiliza na kutenda kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao kama alivyofanya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa! Baba Mtakatifu Ijumaa, tarehe 17 Februari 2017 anatarajiwa kutembelea na hatimaye, kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha “Roma Tre”. Hii itakuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu kukutana kwa mara nyingine tena na vijana wa kizazi kipya kutoka Roma, ili kuwasikiliza na kuwasindikiza katika safari ya maisha yao ya ujana, huku wakiwa na imani na matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.