2017-02-10 15:48:00

Kristo Yesu, dhidi ya sheria tasa isiyokuwa na mashiko!


Asili ya mwanadamu ni mwanajamii. Katika jamii hiyo mwanadamu hawezi kukwepa kuwa na ushirikiano na watu wengine. Hakuna mtu anayeweza kujidai kuishi kama “Gendaeka” , Yule nyani dume anayetembea peke yake porini bila kuwa na mahusiano yoyote na nyani wengine. Daima mwanadamu yupo katika jamii fulani na uhusiana na huyu ama yule na hivyo hujiwekea sheria na taratibu kwa ajili kuleta uelewano, kumpatia kila mmoja haki na wajibu wake au kwa ujumla kuleta uwiano kati yao. Dominika ya hii tunapewa tafakari juu ya dhana hii ya sheria na taratibu katika jamii za wanadamu.

Wazo kubwa linalojitokeza ni juu ya tofauti ya sheria ya Kristo yenye kuzaa matunda na sheria nyingine ambazo huonesha utasa. Sheria na taratibu ni moja ya nyenzo za kuijenga jamii fulani. Watu wanapokutana zaidi ya mmoja ni budi kupeana taratibu ambazo zitamstawisha mtu mmoja mmoja au mahusiahano yao kwa ujumla. Sheria katika ujumla wake inapaswa kumjenga mmoja kuwa bora zaidi katika mahusiano yake na wenzake. Sheria haipaswi kufutwa bila kuwa na faida kwake yeye anayeifuata. Sheria inapaswa kuwa chanzo cha kukua na kumbadilisha mmoja katika mahusiano yake na wengine katika jamii yake husika.

Kristo anajitambulisha kama utimilifu wa sheria zote. Ujio wake katika jamii ya Wayahudi haukuwa na lengo ya kuzitangua sheria ambazo zimekwisha kuwepo tangu awali katika vitabu vya Torati bali amekuja kuitimiliza. Yeye anasema: “haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”. Hili ni onyo dhahiri na namna ya kuwaondoa katika upofu waliokuwa nao. Wao walikuwa wanajikinai kutimiza amri na taratibu wakidhni wamekamilika kumbe waliendelea kudumaa. Sheria na amri walizokuwa wanasisitiza kuzifuata ziligeuka kuwa mzigo na mtego wa kuwanasa wengine waonekane waovu. Amri hizo kwao zimekuwa tasa.

Lengo la Kristo ni kuwafikisha katika mstari ulio sahihi, yaani kutafuta kile kilicho roho au mantiki ya amri yoyote na kukitekeleza. Tofauti na hapo ipo hatari ya kukumbatia sheria na taratibu ambazo badala ya kukujenga basi huishia kukubomoa na pengine kuzidi kujenga ukuta kati yako na wengine. Nia yake Kristo ni kutuepusha na tabia za kiitikadi za siasa kali ambazo badala ya kuujenga ujirani baina ya wanadamu uhuaribu ujirani huo. Mafarisayo na Waandishi walipoteza upendo wa kindugu kwa yeyote ambaye hakuzifuata sheria na amri. Mtu wa namna hii alionekana kuwa najisi na asiye na nafasi katika wokovu.

Sheria au taratibu ambayo haijengi upendo kati ya mtu na mtu hubaki kuwa tasa na mzigo kwa anayeitii. Yoshua bin Sira anatuwekea wazi lililo la muhimu katika kuzishika amri hizo. Jambo la kwanza ni upendo. Yeye anasema: “ukipenda utazishika amri zake”. Tendo hili la kupenda lina mielekeo miwili. Kwanza ni utayari wa yeye ambaye anashika amri. Upendo kwake utamfanya kuwa na hamu na kuifurahia amri inayowekwa mbele yake. Pili ni sababu au kinachokusukuma kupenda. Hapa tunaiona nafasi ya anayeitoa amri hiyo yaani Mungu mwenyewe na anayesababisha amri hiyo itolewe yaani jirani yako. Mmoja anapoutambua ukuu wa Mungu na thamani ya jirani yake ambaye ni ndugu yake basi utaratibu au amri au sheria iwekwayo kwake huipokea kwa furaha na hapo huipenda. Jambo la pili la muhimu kutoka kwa Bin Sira ni uhuru wa mwanadamu katika kuzifuata amri hizi. Ingawa nia na makusudio ya Mungu kuweka taratibu, amri na sheria ni kwa ajili ustawi wa jamii ya wanadamu bado hamshurutishi mtu kutenda haya. Huu ni uthibitisho wa ukuu wa Mungu ambaye huthamini mipango yake na kamwe habadiliki. Yeye mwenyewe ndiye aliyemuumba mwanadamu na utashi huru. Hivyo, pamoja na kwamba amewaka sheria mbele zake uchaguzi unabaki kwake mtu binafsi. Yeye anasema: “mradi hekima ya Bwana inatosha”.

Kristo ndiyo hekima hiyo ya Bwana na utimilifu wa sheria zote. Malumbano yake na Mafarisayo na waandishi (ambao ni wanasheria wa kiyahudi) yalitokana na ukaidi wa kutokumtambua Yeye kama utmilifu wa upendo wa Mungu, Yeye ambaye amekuja kuipatia Torati wanayoishika uhai na kuiondoa katika ufu, kuipatia rutuba na kuindika katika utasa. Wao walijiwekea sheria na taratibu nyingi na hata wakati mwingine kuzifanyia tafsiri bila kuwa na tija katika kumkuza mtu kiutu. Tukichukulia mathalani amri iliyokataza kuua. Kwao Mafarisayo walitazama kitendo cha kuutoa uhai wa mtu mwingine. Hawakujisumbua kuangalia maana yake amri hiyo. Hivyo mmoja hakujali kama amegombana na mwenzake au ana chuki naye au wanadaiana kitu fulani. Mahusiano ya kindugu yanayokuza upendo hayakupewa kipao mbele bali waliitazama tu maana ya moja kwa moja ya amri husika. Hapo ndipo utasa wa amri na taratibu zao ulipolala.

Ninapoambiwa “nisiue” ninaelekezwa katika kuuthamini uhai wa mtu na ndani zaidi ninaelekezwa katika kuuthamini utu. Hivyo katika mjumuiko wa maisha yangu napaswa kutenda yote ambayo yanastawisha utu wa mtu na kuuthamini. Inawezekana kabisa sijawahi kutoa uhai wa mtu lakini ni mchoyo katika kuwa shirikisha wenzangu wahitaji nilivyokirimiwa ikiwemo mali na vinginevyo; mimi ni mnyanyasaji wa watumishi walio chini yangu; au mimi mpangaji wa sera na mipango ya kijamii inayowapora watu wengi wanyonge haki zao za msingi. Mfano leo hii katika dunia kuna vita juu ya utumiaji wa madawa ya kulevya, janga ambalo linamaliza nguvu kazi haswa vijana. Bila kujali thamani ya utu wa mtu na kwa kujikinai kutokuhusika na kosa la kutoa uhai moja kwa moja kwa mkono wako, mmoja atashiriki kwa namna moja au nyingine pengine kwa kuagiza au kutetea waagizaji ili mradi tu yeye aendelee kustawi. Sheria hiyo ya kuua haikukamati lakini upo wapi upendo wako kwa jirani yako? Je, umeoina thamani ya maisha yake na utu wake?

Teolojia ya Kanisa baada ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano na haswa ukichagizwa na hati ya Optatam Totius inajikita katika mrengo huo wa kuikuza roho ya amri na taratibu zote za kibinadamu katika Kristo. Mababa wa Kanisa wanatuambia kwamba: “Majiundo yote ya kiteolojia yanapaswa kupyaishwa katika kulifanya kutaniko dhahiri na Fumbo la Kristo katika historia ya wokovu” (OT n.16). Hili lilikwa jawabu kwa mfumo wa kiteolojia uliokitangulia kipindi hiki ambao ulizingatika katika sheria zilizo kali lakini zenye utasa na zisizomkuza mwanadamu. Tamko mlo ni matokeo ya mapinduzi makubwa yaliyoanzishwa na Mtakatifu Alfonsi Maria Liguori ambaye ni gwiji katika nyaja ya maadili ya kikristo na aliesisitiza sana katika ukuaji wa kikristo kwa kila muumini mmoja mmoja kwa kadiri ya nafasi yake. Kipindi hicho cha nyuma watu wengi walisisitiziwa katika kufuata sheria na taratibu bila kutafuta roho yako na kutafakari ni kipi faida yake katika kukua kiroho.

Ni nafasi ya kujiuliza kila mmoja binafsi swali hili muhimu: Je, sheria na taratibu ninazozifuata zinanisaidia vipi kunikuza katika utu? Je, zinanipeleka katika hali ya kumpenda zaidi Mungu na mwanadamu? Tuepuke kufuata amri au sheria fulani kinafki au kama vipofu. Daima tuitafute roho yake, yaani maana yake na tija yake na kwa njia hiyo tutapa fursa ya kuifurahia, kuikumbatia na kuifanya kuwa mwongozo kwa ustawi wa watu wote katika jamii ya wanadamu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.