2017-02-09 13:38:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani 2017


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuwa mwakilishi wake katika maadhimisho ya Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2017 huko Lourdes, Ufaransa. Maadhimisho haya yatafanyika tarehe 11 Februari 2017 Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Mshangao kwa makuu aliyotenda Mungu: “Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu” Lk. 1:49. Siku hii ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza huko Lourdes kunako tarehe 11 Februari 1993.

Hii ni siku maalum ambayo Mama Kanisa anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa wagonjwa bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Ni wakati wa kusali na kuwaombea wagonjwa na familia zao; kwa kuwaenzi wahudumu katika sekta ya afya pamoja na watu wanaojitolea usiku na mchana kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na wazee sehemu mbali mbali za dunia. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya wito wa huduma, ili kuweza kuwasindikiza wagonjwa na wanaoteseka katika shida na mahangaiko yao. Ni fursa kwa Kanisa kupyaisha tena na tena huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema kwamba, hii ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa. Ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa wakati wa maadhimisho haya huko Lourdes, Ufaransa.

Baba Mtakatifu anapenda kujiweka chini ya Pango la Bikira Maria wa Lourdes, ambaye Mwenyezi Mungu amemtendea makuu na jina lake ni takatifu katika mchakato wa ukombozi wa mwanadamu, kwa kuungana na wagonjwa wote duniani pamoja na familia zao katika sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anaungana pia na familia pamoja na wafanyakazi wote wa sekya afya na wale wanaoendelea kujisadaka usiku na mchana kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na wazee pamoja na kuwatia shime, kuendelea na huduma hii makini kwa ajili ya wagonjwa. Anawataka kuwa na ujasiri wa kumtafakari Bikira Maria, afya ya wagonjwa, ili kuonja ukuu wa huruma ya Mungu kwa kila binadamu pamoja na kujiachilia katika mapenzi yake.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka daima kujipatia kutoka katika imani inayoboreshwa kwa njia Neno na Sakramenti, nguvu ya kumpenda Mungu na jirani hata katika uzoefu na mang’amuzi ya ugonjwa. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Bernadetha aliyeangaliwa kwa jicho la upendo na Bikira Maria kiasi cha kumpokea, kuukubali na kushangazwa na uzuri wake ni kielelezo cha mahusiano ya ndani katika maisha ya binadamu. Bernadetha, maskini, mjinga na mgonjwa anajiona kutazamwa kwa namna ya pekee, kama binadamu na Bikira Maria, anayezungumza kwa heshima na adabu, changamoto ya kutambua kwamba, kila binadamu anapaswa kutendewa namna hii. Wagonjwa na walemavu wanao utu na heshima yao; wanao wajibu na dhamana katika maisha na kamwe hawawezi kugeuzwa na kuwa kama vichokoo hata pale wanapoonekana kuwa hawajitambui tena!

Bernadetha baada sala pale kwenye Pango la Bikira Maria, udhaifu wake ukageuka kuwa ni mhimili na nguzo kwa ajili yaw engine, kiasi kwamba upendo wake ukageuka kuwa ni utajiri kwa jirani pamoja na kujisadaka kwa ajili ya wokovu kwa binadamu. Bikira Maria alimwomba asali kwa ajili ya wadhambi, jambo linalowakumbusha waamini kwamba, wagonjwa na walemavu wanayo kiu na ari ya kutaka kuishi Ukristo wao, kiasi cha kujitosa bila ya kujibakiza kama wafuasi wamissionari wa Kristo Yesu. Bikira Maria alimkirimia Bernadetha wito wa kuwahudumia wagonjwa, kiasi cha kutambulikana kama Dada wa upendo, utume wa hali ya juu kabisa unaomfanya kuwa ni mfano bora wa kuigwa na rejea kwa wafanyakazi wote katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuomba neema kutoka kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili kuweza kuwa na mahusiano mazuri na mgonjwa, ambaye kimsingi anahitaji msaada hata wakati mwingine kwa mambo ya kawaida kabisa, lakini ndani mwake anabeba zawadi ambayo anaweza kushirikishana na wengine.

Sura ya Bikira Maria, faraja ya wagonjwa inauangazia uso wa Kanisa katika dhamana na wajibu wake wa kila siku kwa ajili ya wagonjwa na maskini, kiasi kwamba, matunda ya utume huu wa Kanisa ni sababu msingi ya shukrani kwa Kristo Yesu, aliyejishikamanisha na binadamu kama kielelezo cha utii wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, kiasi hata cha kufa Msalabani, ili kuwakomboa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mshikamano wa Kristo Yesu, Mwana wa Bikira maria ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ukuu wa huruma ya Mungu inayojionesha katika maisha ya binadamu, hasa pale maisha yanapotikiswa kwa magonjwa, madonda, dharau, kutengwa na kubezwa pamoja na mahangaiko. Kristo Yesu anawapatia waamini matumaini ya kusimama pamoja na kuendelea kuwategemeza.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, utajiri mkubwa wa ubinadamu na imani usipotee hivi hivi na badala yake uwasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuweza kupambana na udhaifu wa kibinadamu pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza, ili kujenga na kudumisha utamaduni unaoheshimu na kuthamini utimilifu, utu na heshima ya binadamu. Kuna haja ya kuwepo na mtazamo makini kuhusiana na masuala ya maadili kibaiolojia, huduma kwa wagonjwa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anasema, katika maadhimisho ya Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2017 anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya Sala na Sadaka yake; ili kuwaenzi wafanyakazi katika sekta ya afya; watu wa kujitolea pamoja na watawa ambao wamekuwa mstari wa mbele kwa huduma kwa wagonjwa na wazee sehemu mbali mbali za dunia. Papa anasema, anaungana na taasisi za Kanisa na Serikali zinazotoa huduma kwa wagonjwa; bila kuzisahau familia zinazowahudumia wagonjwa kwa upendo na ukarimu.

Wote hawa, Baba Mtakatifu anawaombea ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uwepo wa upendo wa Mungu pamoja na kuendelea kuiga mfano wa mashuhuda na marafiki wa Mungu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Kati yao ni Mtakatifu Yohane wa Mungu, Mtakatifu Camillo wa Lellis, Msimamizi wa Hospitali na wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na Mama Theresa wa Calcutta, Mmissionari wa wema wa Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 25 ya Wagonjwa Duniani kwa kumwomba Bikira Maria awasaidie waamini kuwa na matumaini, udugu na uwajibikaji kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu, furaha shukrani kwa kuwa waaminifu kwa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.