2017-02-08 09:35:00

Papa Francisko: Angalieni kuna maskini wanaobisha hodi malangoni penu


Changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni kujitahidi kumwilisha sehemu ya Injili ya Lazaro maskini na tajiri asiyejali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zake. “Neno ni zawadi; jirani yako ni zawadi pia”. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2017, muda wa kusali, kutafakari, kujikita katika maisha ya Kisakramenti, lakini zaidi kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji!

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni mia nane wanaosumbuliwa kwa baa la njaa na utapiamlo mkali; kuna watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, dunia hii imegubikwa na umaskini wa kiroho na kimwili; umaskini wa hali na kipato! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2017 ni changamoto kubwa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa jirani zao, kwani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya yamesemwa na Monsinyo Giampietro Dal Toso, Katibu mwakilishi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu,  Jumanne tarehe 7 Februari 2017 wakati wa kuwasilisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2017, huku akiwa ameambatana na Chiara Amirante, mwanzilishi wa Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti”.

Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka uliokubalika kwa waamini kufungua malango ya nyoyo zao kwa maskini ili kutambua Uso wa Kristo Yesu, tayari kukutana naye katika hija ya maisha ya kiroho. Kila mtu wanayekutana naye ni zawadi inayopaswa kupokelewa, kuheshimiwa na kupendwa. Neno la Mungu liwasaidie waamini kupokea na kupenda zawadi ya maisha, hususan pale mtu anapokuwa dhaifu na maskini. Ili kumwilisha changamoto hii, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha ya yule mtu tajiri. Kimsingi dhambi inawafumba macho waamini kiasi cha kutoweza kuona wala kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 anakazia sana umuhimu wa Neno la Mungu na hasa mfano wa tajiri na Lazaro maskini, uwasaidie waamini kujiandaa barabara kwa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Liturujia ya Kupakwa majivu, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, waamini watapakwa majivu na kukumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena. Maskini na matajiri wote watakufa tu na wala hawatachukua jambo lolote kutoka hapa duniani. Monsinyo Giampietro Dal Toso anasema, tajiri anayesimuliwa katika sehemu ya Injili ya Luka anashutumiwa si kwa sababu alikuwa na mali na utajiri mkubwa, lakini ni kwa sababu alishindwa kuona, kutambua na kuguswa na mahangaiko ya Lazaro maskini, ni mtu aliyefungwa macho na utajiri na ubinafsi wake.

Kwa upande wake, Chiara Amirante, mwanzilishi wa Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” anakazia kwa kusema, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini ambao ni amana na utajiri wa Kanisa; kwa kuwasikiliza na kujibu kilio chao cha ndani. Katika maisha na utume wake, amekutana na kugundua aina mpya za umaskini wa kiroho na kimwili zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Matumizi haramu ya dawa za kulevya; ulevi wa kupindukia; biashara ya ngono; watoto walionyanyaswa kijinsia bila kusahau makundi ya wasichana wanaojitesa kwa ajili ya kutafuta ulimbwende na matokeo yake wanadhohofisha afya zao kiasi hata cha kuchungulia kaburi!

Chiara Amirante anasema baada ya kuonja changamoto hizi, akagundua kwamba, kulikuwa kuna haja ya kujenga madaraja ya watu kukutana na kumwilisha changamoto hizi za maisha katika mwanga wa Injili. Leo hii Jumuiya ya “Nuovi Orizzonti” ina vituo 207 kwa ajili ya kuwapokea na kuwahudumia maskini hawa pamoja na kuwapatia majiundo endelevu katika maisha yao. Kuna umati mkubwa wa maskini waliosaidiwa sasa wanaishi maisha mapya kabisa na wao wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.