2017-02-04 16:23:00

Ukristo ni kuishi na wala si kuishia! Ni ushuhuda wenye mvuto!


Yaani mimi sipati picha kabisaa! Dominika iliyopita tulipanda mlimani ambako tulikabidhiwa Katiba mpya ya Yesu. Tukabaki tumeachama midomo tukiishangaa jinsi ilivyo ngumu kueleweka na kuitekeleza. Lakini kama mtu anaipokea na kuitekeleza, maisha yake mtu huyo yanakuwa ya pekee na tofauti na yale ya kawaida. Kishawishi kikubwa cha maisha ya kawaida ni kile cha kutaka kujikomboa wenyewe. Ukifanya hivyo hutofautiani na Wabudha wanaotarajia kuangaziwa na kujipatia utakatifu na furaha ya binafsi wanayoiita nirvana. Kumbe mtu anayeiishi Katiba ya Yesu inakukomboa binadamu mzima. Hii ni Katiba mbadala, dhidi ya thamani zilizoko katika katiba wanayoshika watu wa ulimwengu huu. Leo Yesu anatushusha kutoka mlimani tulikokuwa na kutupeleka bondeni kwenye mazingira ya watu wa kawaida wanaofuata maisha kadiri ya vigezo vyao. Huko ndiko tunatakiwa kuiishi katiba ya Yesu kati ya watu hao. Anatuletea ujumbe katika picha mbili za jinsi ya kuwajibika katika mazingira hayo tutakayoishi.

Mosi anasema: “Ninyi ni chumvi ya dunia.” Kazi ya kwanza ya chumvi ni kunogesha, kuleta radha au utamu katika chakula. Lakini  chumvi inanoga kama imeyeyuka na kuchanganywa vizuri na chakula. Kwa hiyo ujumbe wa kwanza tunaopata ni kwamba mkristu hatakiwi kutoroka ulimwengu, bali ajichanganye nao. Kisha aleteshe radha au utamu wa maisha. Radha na utamu huo ujioneshe na kudhihirika katika mazungumzo yetu. Paulo anasema: Mazungumzo yenu yawe yameungwa au yawe yananoga chumvi (Kolosai 4:6). Kumbe kinyume chake maneno yetu yanaweza kuwa matupu yasiyo na lolote, yasiyo na uzito. Kama tunavyosema “maneno matupu hayavunji mfupa.”

Mdomoni mwa mkristo hakutakiwi  kutoka lugha chafu utadhani chereheani! Lugha ya uwongo na udanganyifu, bali budi kuwa na lugha inayonoga yenye radha yaani yenye kuleta maana ya maisha ya binadamu. Mtu asiye na chumvi yenye utamu wa kiinjili, lugha yake inatoa furaha ya muda mfupi, kama vile furaha ya kufaulu mtihani wa kidato cha nne, au wa kidato cha sita, furaha ya kufuzu chuo kikuu, au ya kufunga ndoa, au ya kuwa na kazi nzuri, ya kupata mshahara mzuri, na kufanikiwa katika maisha ya hapa duniani nk. Furaha hizi zote ni nzuri na zinafaa, lakini zina kikomo chake kwa sababu baadaye mtu anajiuliza mwisho wa maisha yake aliyoishi ni upi. Kwamba maisha yangu yana mwelekeo gani zaidi ya hapa nilipofika. Hapo ndipo anapohitajika chumvi ya mkristu, kwa sababu inatia utamu, yaani inaletesha maana ya maisha ya binadamu.

Pili, chumvi inahifadhi chakula kisioze. Kutoka miaka elfu mbili kabla ya Kristu watu walihifadhi vyakula kwa kutumia chumvi. Hapa Yesu alipata mang’amuzi zaidi kutoka kwa wakazi wa Magdala. Watu wa Magdala walikuwa wanakausha na kuhifadhi samaki kwa kutumia chumvi ya kutoka bahari ya chumvi. Maana hii ya kuhifadhi anayomaanisha Yesu ni kwamba baada ya kushuka kutoka mlimani mkristu yabidi afanye juu chini kuzuia uozo wa kila aina. Ajitahidi kuona kwamba katika jamii aliyopo haiharibiki na kuoza. Kwa vyovyote jamii ikiendelea kuongozwa na binadamu waovu, ni rahisi sana kuchanganya mambo na kuozesha maisha. Mfano, kama thamani za msingi katika jamii  zimelala katika uzalishaji tu, katika pesa na utajiri hapo utu wa ubinadamu unadhalilishwa kama ilivyokuwa wakati wa nabii Amosi. Binadamu alikuwa na thamani ya katambuga, au wakati wa Yesu ambapo kondoo alithaminiwa zaidi ya binadamu. Kumbe binadamu anashika nafasi ya kwanza katika maisha kuanzia anapozaliwa hadi atakapokufa. Kwa hiyo mkristu yabidi aone maisha ya binadamu kuwa matukufu na matakatifu yasivurugwe na thamani zozote zile za ulimwengu huu, bali mambo yafanyike kadiri ya mapendekezo ya Kristu mlimani.

Tatu, chumvi ilitumika katika karamu ya kufunga agano, mkataba, makubaliano, au mapatano, ya urafiki. Kadhalika Mungu alitoa sheria za sadaka alipofunga agano na Israeli. Hapo walikula mkate nachumvi. Chumvi iliyotumiwa kwa sadaka iliitwa “chumvi ya Agano” (Law. 2:13.) Hapo ilimaanisha kuwa ni agano lisiloweza kuvunjwa wala kwisha kwa namna yoyote ile. Kwa hiyo mkristu ni chumvi kwa sababu anatoa ushuhuda wa uaminifu wa agano alilofanya na Yesu, mbele ya ulimwenguni mpya wa upendo wa Mungu usiovunjika wala kuanguka. Mkristu asipotoa ushuhuda kwa uaminifu huo anapoteza radha ya ukristu. Neno lililotumika la kupoteza radha ni moraino (moranthe) lenye maana ya kutokuwa na hamu, kutofaa.

Picha ya pili Yesu anasema: “Ninyi ni mwanga wa ulimwengu.” Kwa Wayahudi mwanga ulikuwa wa Tora (kitabu cha Mungu). Ndani ya Hekalu la Yerusalemu kulikuwa na pazia lililotenga sehemu ya patakatifu na patakatifu pa patakatifu. Hapo katikati kulikuwa na kinara cha myenge kilichoitwa menora. Kilionesha kwamba kutoka patakatifu pa patakatifu hutokea Neno la Mungu (Tora) ambayo ni mwanga wa ulimwengu. Yesu anasema, hakuna tena Tora nyingine itakayotoa mwanga, bali sasa mwanga huo budi uwe ni maisha yenu yanayotakiwa yaangaze kutokana na Injili mnayoishi. Ninyi ndiyo mwanga wa ulimwengu. Kazi ya mwanga kusaidia kuona vizuri. Kama katika kutembea mwanga unakusaidia kuona njia na kuchagua pahala pa kukanyaga au kupita. Kadhalika katika kununua vitu dukani, mwanga unakusaidia kupambanua bidhaa na kuchagua kilicho kizuri na kisicho kizuri cha kununua. Kwa hiyo mwanga ni alama ya upambanuzi na uchaguzi wa mambo mema na mabaya, au uchaguzi wa maisha ya kiutu na yasiyo ya kibinadamu. Binadamu yabidi apokee mwanga huo siyo tu kwa macho bali hata kwa masikio na kuuhifadhi katika sakafu ya moyo wake, ili umsaidie kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Mwanga huo yabidi uonekane vizuri, “watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango.” Yaani mwanga huo usifunikwe na kikapu. Chombo hiki kilikuwa ni kipimo cha kupimia ngano kama ilivyo pishi. Yesu anasema yabidi watu wote wauone mwanga wenu, yaani watu wajue uzuri wa maisha yenu. Kwa hiyo, kufunika mwanga chini ya pishi maana yake ni kuitangaza kadiri ya vipimo vyenu (pishi) vya kufikiri. Kila mmoja anayo namna yake ya kufunika vipengee muhimu vya mapendekezo ya Yesu ya Injili. Yesu anatuambia tusifanye hivyo, yaani tusichanganye mwanga wa Injili na myanga mingine ya ufunuo inayoibuka hapa na pale kama uyoga. Tusiufunike mwanga wake chini ya pishi au fikra zetu finyu, bali tuache umulike wenyewe mubashara! Kwa wale wanaotaka kujikumbushia umombo eti ni “Live”.

Aidha, Yesu anasema: “Mwanga uwaangaze wote waliomo nyumbani.” Inabidi kwanza mwanga huo tuangaze ndani mwetu kabla ya kuwaangazia wengine. Tena anasema “ili watu wapate kuyaona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” Kwamba yabidi maisha yetu sisi wenyewe yawe kwanza mwanga, ili yaweze kuangaza wengine. Mkristu asiwe hamnazo juu ya kile ambacho ulimwengu unavyomfikiria yeye. Kwamba wakristu wawe tayari kukosolewa, na pengine hata kudhulumiwa kwani mwanga unawachokoza wale wasioishi kiutu. Kwa hiyo ujumbe wa Injili ya leo ni huu kwamba maisha ya mkristu siyo ya kulazimishana, hayafanyi matangazo ya kibiashara, bali ni kuishi. Ukristo maana yake kuishi, na kutoa ushuhuda wa maisha katika ulimwengu kama ilivyo chumvi na mwanga.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.