2017-02-04 08:14:00

Kardinali Parolin: Congo Brazzaville: huduma, ustawi na mafao ya wengi!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, baada ya safari yake ya kikazi nchini Madagascar kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar, tarehe 1 Februari 2017 ameandoka Madagascar kuelekea Congo Brazzavile ili kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 40 ya uhusiano wa kidiplomasia na Congo Brazzavile. Amepata pia fursa ya kusimama kidogo Nairobi, Kenya, na hivyo kukutana na Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini, aliyemtaarifu hali ya kisiasa na kijamii ilivyo kwa sas anchini Kenya.

Awamu ya pili ya ziara ya Kardinali Parolin, imemwezesha kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville, ili kuzungumza kwa kina na mapana kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini humo, fursa na changamoto wanazokabiliana nazo Maaskofu pamoja na dhamana ya Kanisa nchini humo katika mchakato wa kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Congo Brazzaville. Alipowasili, Brazzaville, Jumatano tarehe 1 Februari 2017 amepokelewa na viongozi wa Serikali chini ya Bwana Clemente Moumba, Waziri mkuu wa Congo, Brazzaville pamoja na viongozi wa Kanisa wakiongozwa na Askofu mkuu Francisco Escalante Molina, Balozi wa Vatican nchini Jamhuri ya Watu wa Congo Brazzaville. Askofu Daniel Mizonzo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville ameiongoza familia ya Mungu nchini humo ili kumlaki Kardinali Pietro Parolin, wakati wa hija yake ya kikazi nchini Congo Brazzaville.

Maaskofu tisa wamepata nafasi ya kuzungumza kwa kina na mapana na Kardinali Parolin kuhusiana na maisha na utume wao changamoto, fursa na vipaumbele katika mchakato wa shughuli za kichungaji na kitume nchini humo bila kusahau masuala ya kisiasa kwani yanaligusa pia Kanisa. Maaskofu wameshauriwa kufuatilia utekelezaji wa Itifaki ya Ushirikiano mara baada ya kutiwa mkwaju sanjari na kuhakikisha kwamba, Maaskofu wanaendelea kudumisha mahusiano mema sanjari na kufuatilia utekelezaji wake.

Mchakato huu utekelezwe kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kardinali Parolin amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kujikita katika mchakato wa majiundo ya awali na endelevu kwa waamini walei li kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, waweze kuyachachua malimwengu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kardinali Parolin amepata nafasi pia ya kusikiliza hali tete inayoendelea kuwaandama wananchi wa Congo Brazzaville pamoja na nchi jirani ya DRC. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville kwamba, mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Kardinali Emile Biayenda aliyeuwawa kikatili miaka 40 iliyopita utaweza kufanikiwa. Hali ngumu ya uchumi, umuhimu wa kuwa na kituo cha huduma ya tiba kwa wakleri na watawa ni mambo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville wakati wa kikao chao na Kardinali Pietro Parolin.

Tarehe 2 Februari 2017, Kardinali Pietro Parolin akiwa ameambatana na Askofu mkuu Anatole Milandou pamoja na Askofu mkuu Francisco Escalante Molina, Balozi wa Vatican nchini Jamhuri ya Watu wa Congo Brazzaville wamemtembelea Bwana Jean Claude Gakosso, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Serikali inaridhishwa na mchango unaotolewa na Mama Kanisa katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii.

Ameridhishwa na mchango wa Kanisa  katika kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani, utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Serikali inafikiria uwezekano wa kufungua ubalozi wake mjini Vatican. Kwa upande wake, Kardinali Parolin amekumbushia umuhimu wa Itifaki ya Makubaliano itakayosaidia kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na Kanisa pamoja na kutoa huduma kwa familia ya Mungu nchini humo pasi na ubaguzi. Wamegusia pia hali halisi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Ukanda huu na hatimaye, kubadilishana zawadi.

Kardinali Parolin na ujumbe wake, walikutana na kuzungumza pia na Bwana Clemente Moumba, Waziri mkuu wa Congo, Brazzaville. Hapa wamezungumzia kuhusu Itifaki ya Makubaliano; hali ya uchumi, kisiasa na kijamii nchini humo pamoja na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji Barani Afrika; hali ya usalama na amani eneo la Maziwa Makuu na kwamba, Serikali inaendelea kupambana na wapiganaji wa msituni, ili kuhakikisha kwamba, amani, usalama na utulivu vinarejea tena nchini humo. Hapa mkazo ni majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Waziri mkuu wa Congo, Brazzaville ametumia nafasi hii kumwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini yao. Amegusia pia hali ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanaoanza kurejea tena makwao. Kardinali Parolin amepata nafasi pia ya kutembelea: Kituo cha huduma cha Watoto walemavu cha Mtumishi wa Mungu Kardinali Emile Biayenda, Kituo cha kulelea watoto wadogo, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi cha Accuel Bèthanie.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.