2017-02-03 13:42:00

Familia ni kitovu cha Uinjilishaji!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ni kati ya Mababa wa Sinodi walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi mbili za familia na matunda yake ni Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Ngalalekumtwa anasema, familia ni kitovu cha Uinjilishaji mpya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, familia kama ilivyokuwa hata kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mahali muafaka pa kutekelezea mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Familia ni shule ya utakatifu, haki, amani, upendo na mshikamano. Hapa ni mahali ambapo waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kusimama kidete kupinga na kupambana na maovu yanayoizunguka Jumuiya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Yaani: ubinafsi, kutojali wala kuthamini utu na heshima ya binadamu; sheria na kanuni maumbile kadiri ya mpango wa Mungu kwa maisha ya binadamu.

Kutokana na changamoto zote hizi, inakuwa vigumu familia kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kuna watu wametopea katika malimwengu kwa kujikita katika ukanimungu. Hawako tayari kutekeleza Amri za Mungu katika maisha yao kwani wanadhani kwamba, wanaweza hata kuishi bila ya uwepo wa Mungu. Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ubinafsi na kiburi cha mwanadamu aliyejikuza na hivyo kuwa kikwazo cha utangazaji na ushuhu wa Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, jitihada za Uinjilishaji hazina budi kupata chimbuko lake katika tunu msingi za maisha ya kifamilia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.