2017-02-02 14:57:00

Makanisa yanataka kuwekeza katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani


Wajumbe wa ofisi ya majadiliano ya kidini na ushirikiano kutoka katika Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na wafanyakazi kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, Jumanne, tarehe 31 Januari 2017 walihitimisha mkutano wao wa siku mbili uliokuwa unafanyika mjini Roma. Wajumbe hawa wameridhishwa na mkutano wao ambao umefanyika siku chache tu baada ya kuhitimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo ambalo kwa Mwaka 2017 limeongozwa na kauli mbiu “Upatanisho: Upendo wa Kristo unatuwajibisha”.

Wajumbe, wanapenda kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani kwa urafiki na ushirikiano wa dhati unaoendelea kujionesha kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mahusiano kati ya watu binafsi na jumuiya za waamini wa dini mbali mbali duniani. Wajumbe walikutanika ili kuandaa muswada wa waraka wa pamoja juu ya ujenzi wa “Elimu ya amani” pamoja na kuibua miradi mbali mbali ya ushirikiano kama ilivyojitokeza kwa miaka iliyopita. Wajumbe walipata nafasi ya kuweza kubadilishana: uzoefu na mang’amuzi ya utume wao katika kipindi cha mwaka 2016 pamoja na kujiwekea mikakati ya kufanyia kazi kwa mwaka 2017. Kimsingi wameridhia mchakato wa kuendelea kushirikiana kwa dhati ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa kwenye ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.