2017-02-02 15:14:00

Familia ni chemchemi ya furaha ya upendo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasema, litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia katika maisha na utume wake, lakini zaidi pale ambapo tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ziko hatarini. Haya yamo kwenye barua ya kichungaji iliyoandikwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe kwa familia ya Mungu nchini humo ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoyo, matatizo na fursa katika maisha na utume wake.

Kanisa linawashukuru, linawasifu na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujizatiti katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, licha ya changamoto zilizopo kwa sasa yaani kinzani za kisiasa, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na athari za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Barua hii ya Maaskofu Katoliki Zimbabwe inachota utajiri wake kutoka kwenye maamuzi yaliyofanywa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, Sinodi za Maaskofu Katoliki kuhusu familia na hatimaye, Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” ambao kwa sasa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa familia.

Wanandoa na familia wanakumbushwa kwamba, upendo ni kiini cha maisha ya ndoa na familia na ni chemchemi ya furaha, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia sehemu mbali mbali za dunia. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mkutano wake uliofanyika nchini Angola, lilitoa ujumbe wa matumaini na mshikamano kwa familia ya Mungu Barani Afrika, changamoto ya familia Barani Afrika kuwa ni chombo na mashuhuda wa furaha ya familia, utakatifu na madhabahu ya maisha ya mwanadamu tangu anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Wanandoa wanahamasisha na Kanisa kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo kwa kushuhudia Injili ya uhai. Katekesi makini juu ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia inapaswa kutolewa kwa waamini, ili waweze kuifahamu na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao na kamwe wasiwe ni bendera kufuata upepo. Waamini watambue wajibu na dhamana yao, wawe tayari kuutekeleza kama kielelezo cha imani na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kujikita katika kanuni maadili na utu wema, chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, ili hatimaye, kuwa na furaha ya maisha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Wanandoa na familia wanahimizwa kuwa ni vyombo vya neema na faraja; furaha, amani, upendo na mshikamano wakati wa raha na huzuni, hadi kifo kitakapowatenganisha. Kanisa kwa upande wake liendelee kuwa karibu na familia zinazoogelea katika shida na magumu, wasi wasi na hali ya kukata tamaa ili kuzijengea tena matumaini ya kuanza upya katika Kristo Yesu, huku wakichukua vyema Msalaba wao na kumfuasa. Wanandoa watarajiwa wafundwe barabara ili wafahamu mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia, ili hatimaye, waweze kuwa kwelini ni mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia, badala ya kuwa ni watalii wa maisha ya kifamilia, kiasi kwamba, wanapotikiswa, wanaanguka na kusambaratika kiasi cha kupoteza dira na mwongozo wa Injili ya familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke, ili waweze kusaidiana na kukamilisha na hatimaye, kufikia utakatifu na maisha ya uzima wa milele. Wote wana utu sawa mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini wameumbwa tofauti ili kukamilishana. Ndoa za watu wa jinsia moja, si mpango wa Mungu kwa binadamu ni kinyume cha maadili na utu wema. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa vyema katika masuala ya ndoa na familia, ili wasimezwe na malimwengu na kujikuta wakishabikia ndoa za watu wa jinsia moja. Upendo wa kweli katika maisha ya ndoa na familia, ni chemchemi ya furaha, amani na matumaini. Watoto ni matunda ya furaha na upendo ndani ya familia. Kumbe, wazazi wa pande zote mbili wanapaswa kuwajibika katika makuzi na malezi ya watoto wao, ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi wanasema Maaskofu Katoliki Zimbawe katika barua yao ya kichungaji kuhusu Injili ya familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.