2017-02-02 15:50:00

Askofu mkuu Ruwaichi: Kanisa linawahitaji watawa wakakamavu!


Mama Kanisa tarehe 2 Februari 2017 anaadhimisha Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 21 ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II ili kuwaenzi watawa duniani kutokana na mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo! Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kuwaombea, kuwaenzi na kushikamana na watawa katika maisha na utume wao.

Askofu mkuu Ruwaichi anawaalika waamini kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maisha ya watu wa wakfu. Hawa ni Manabii wa Kristo Yesu na wito wao ni kumfuasa, kumtumikia na kumshuhudia Kristo Yesu aliyekuwa mtii, fukara na mwenye usafi kamili wa moyo. Watawa kwa njia ya utashi wao kamili wanajifungamanisha na Kristo kwa njia ya mashauri ya Kiinjili, maarufu kama nadhiri katika Mashirika yao ya Kitawa na Kazi za Kitume.

Askofu mkuu Ruwaichi anasikitika kusema kwamba, hizi ni nyakati zenye changamoto nzito, kiasi kwamba, watawa wanaweza wakasahau na kupuuzia wito wao wa msingi na kujikita kwamba, badala ya kutakatifuza malimwengu kwa njia ya wakfu na ushuhuda wao, wakajikuta wanaburuzwa na kumezwa na malimwengu. Watawa kwa mara nyingine tena, wanaalikwa kuvumbua ule upendo wao wa awali, wadumu katika furaha na kujitahidi kuishi kwa uaminifu, upendo huku wakipania kuzamia zaidi katika maisha na wito wao.

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, katika zama hizi za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Kanisa linawahitaji watawa wakakamavu katika mambo matakatifu. Wawe makini na wakomavu kutumia maendeleo ya sayansi nateknolojia; wayakumbatie kwa kiasi, uwajibikaji sanjari na kuzingatia karama za Mashirika yao, vinginevyo wanaweza kujikuta wanashindwa kukumbatia mashauri ya Kiinjili katika maisha ya kijumuiya, kwani kila mtawa atajikuta akiwa anaogelea katika ulimwengu wake binafsi! Hizi ni zama za ubinafsi wa kupindukia, kumbe watawa wanapaswa kuwa macho na makini!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, anahitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kusema kwamba, Kanisa litaendelea kuwakimbusha wajibu wao katika maisha na wito wa kitawa; litawatia shime kusonga mbele pasi na wasi wasi katika maisha na utume wao na kwamba, litaendelea kushikamana nao ili kuishi zawadi na kutumia vyema wito wao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.