2017-02-01 15:22:00

Yanayoendelea kujiri kwenye ziara ya Kardinali Parolin Barani Afrika


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anaendelea na ziara yake ya kwanza ya kikazi Barani Afrika, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Madagascar. Jumatatu, tarehe 30 Januari 2017 ametoa mhadhara kuhusu “Dhamana ya diplomasia ya Vatican mintarafu hali ya kimataifa kwa wakati huu”. Vatican inaendelea kutekeleza dhamana hii kama sehemu ya utume wake kwa Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii, ili kuwa na amani itakayochochea mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na mapambano dhidi ya majanga asilia yanayoendelea kumwandama mwanadamu kila kukicha!

Kardinali Parolin amegusia changamoto ya majanga asilia kama vile ukame wa kutisha na baa la njaa ambalo kwa muda wa miaka mitatu, lilitikisa na kupigisha magoti nchi ya Madagascar, lakini kama kawaida, waathirika wakuu walikuwa ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”.  Mhadhara huu ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali kutoka Madagascar, Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini Madagascar, Wakleri na Watawa na waamini katika ujumla wao.

Amesema, Kanisa Katoliki linaipongeza Serikali ya Madagascar kwa kusimama kidete katika kukabiliana na changamoto zote hizi na kwamba, kuna haja ya kuendelea kujizatiti katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi pamoja na kusimama kidete kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha, mila desturi na tamaduni za wananchi wa Madagascar. Wananchi wa Madagascar wanatambua kwamba, amani na usalama ni chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya binadamu bila kusahau mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayozingatia mahitaji msingi ya binadamu.

Kardinali Parolin anaendelea kukaza kwa kusema, Jiografia ya Madagascar inaiwezesha nchi hii kuwa ni daraja la watu wenye tamaduni, imani na makabila tofauti kuweza kukutana na kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Tofauti zao msingi ziwe ni sehemu ya utajiri wa wananchi wa Madagascar. Sera na mikakati ya maendeleo haina budi kwanza kabisa kuibuliwa na wananchi wenyewe ili waweze kuitekeleza kwa ari na moyo mkuu. Utamaduni wa Kabary, maarufu sana nchini Madagascar, umempatia nafasi Kardinali Parolin kuzungumzia kuhusu diplomasia ya Vatican chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Mkazo ni kujikita katika hekima, heshima, kanuni maadili na kiasi kama sehemu muhimu sana ya utamaduni wa Kabary.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 29 Januari 2017 baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican alikwenda moja kwa moja hadi mjini Addis Ababa, Ethiopia ili kushiriki katika mkutano wa Wakuu wa 28 wa Wakuu wa Umoja wa Afrika. Katika mkutano huu, Bwana Moussa Faki Mahamat kutoka Chad amechaguliwa kuwa ni Kamishina wa Umoja wa Afrika. Kwa mara ya kwanza Mfalme Mohammed V kutoka Morocco ameshiriki baada ya Morocco kujitenga kwa takribani miaka 33 kutokana na mgogoro wa Sahara Magharibi. Umoja wa Mataifa umezitaka nchi za Kiafrika kufungua malango ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaokimbia vita, vurugu, mipasuko ya kijamii na majanga asilia. Viongozi wa Umoja wa Afrika wamegusia pia mageuzi yatakayouwezesha Umoja kujitegemea kwa rasilimali fedha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.