2017-02-01 15:40:00

Watawa saidianeni kuboresha maisha na utume wenu ughaibuni!


Padre Felix Mushobozi, C.PP.S. wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania, hivi karibuni alimwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, toba na kuomba neema kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre. Kilele cha maadhimisho haya kilikuwa ni hapo tarehe 8 Novemba 2016 aliposhiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. 

Hivi karibuni akizungumza kwenye mkutano wa Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma mjini Roma, Padre Mushobozi aliwataka wakleri na watawa kukumbukana na kusindikizana katika sala na sadaka zao, ili waweze kudumu katika maisha na wito wao kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yao. Amewataka watanzania kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati wakati wa raha na magumu; pamoja na kuendelea kutiana shime katika huduma mbali mbali wanaozitekeleza kama wanafunzi na walezi.

Amekazia umuhimu wa ushirikiano na mawasiliano ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa watanzania, hasa wanapokuwa huku ughaibuni kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu! Kwa namna ya pekee, amewataka wakleri na watawa kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha yao: kiroho, kiutu na kiakili, ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa, hasa wakati huu wanapokuwa ughenini. Wasaidiane na kujengana katika maisha ya Kisakramenti hasa Sakramenti ya Upatanisho pamoja na ushauri makini kwa kuzingatia mipaka na nafasi ya kila mtu. Kipindi hiki cha masomo na utume nchini Italia, iwe ni nafasi ya kujichotea hekima, ujuzi na maarifa, mambo msingi yatakayosaidia katika mchakato wa ujenzi wa Taifa na Kanisa la Tanzania katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.