2017-02-01 14:38:00

Papa Francisko: Matumaini ni chemchemi ya furaha, nguvu na imani!


Matumaini ya Kikristo ni fadhila ya unyenyekevu na nguvu inayowategemeza Wakristo katika maisha na utume wao, kiasi hata cha kuweza kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Matumaini ni chemchemi ya furaha inayoshibisha nyoyo za waamini na amani tele. Waamini kamwe wasikubali kupokwa fadhila ya matumaini katika maisha yao! Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe1 Februari 2017 kwenye Ukumbi wa Paulo VI.

Baada ya kuchambua kwa kina na mapana kuhusu fadhila ya matumaini ya Kikristo mintarafu Agano la Kale, Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua matumaini ya Kikristo mintarafu mwanga wa Agano Jipya unaofumbatwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; chimbuko la Fumbo la Pasaka, mwaliko kwa waamini kukesha, kuwa na kiasi na hatimaye, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka; kwa kujivika imani na upendo na chapeo yao iwe ni tumaini la wokovu. Hiki ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayotangazwa kwa mara ya kwanza kwenye Jumuiya ya Wathesalonike, iliyokuwa imeundwa hivi punde.

Licha ya magumu, changamoto za maisha na majaribu, bado iliweza kusimama kidete katika imani na kuadhimisha kwa kishindo Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Wakristo waliozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu wanakuwa ni watoto wa mwanga kwa kuungana na Kristo Yesu, sababu ya furaha ya Mtakatifu Paulo! Fumbo la Pasaka ni tukio la pekee linalojikita katika maamuzi ya historia na maisha ya kila mwamini. Waamini hawa walikuwa wanatatizwa na imani juu ya Ufufuko wa wafu na wala si juu ya ufufuko wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Fumbo la kifo ni changamoto ya kiimani inayowataka waamini kurejea tena katika msingi wa imani ili kutambua kazi ya ukombozi ambayo Mwenyezi Mungu ametenda kwa njia ya Kristo Yesu kwa ajili ya waja wake. Katika shida na mahangaiko ya imani, Mtakatifu Paulo anawataka waamini  katika majaribu na magumu ya maisha kuhakikisha kwamba wanajikita katika tumaini la wokovu na haya ndiyo matumaini ya Kikristo ambayo tayari yamekwisha kutekelezwa na yataendelea kutekelezwa katika maisha ya kila mwamini.

Ufufuko wa wafu anakaza kusema Baba Mtakatifu ni ukweli mtupu unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Kumbe, matumaini maana yake ni kujifunza kuishi matarajio haya, kwa kuwa na unyenyekevu na umaskini wa roho, kwani mtu anayedhani kwamba, anajitosheleza na kujiamini hawezi kuwa na matumaini kwani anajitumainia mwenyewe! Waamini wanakumbushwa kwamba, Yesu Kristo ameteswa na kufa kwa ajili yao, ili waweze kuishi pamoja naye.

Haya ni maneno ya faraja na amani, ndiyo maana Kanisa linawahamasisha waaamini kusali kwa ajili ya kuwaombea Marehemu wao waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu, ili waweze kuungana na Kristo Yesu, na kuishi pamoja naye milele yote. Haya ni matumaini waliyokuwa nayo hata Waisraeli katika Agano la Kale. Ndiyo maana Ayubu anasema kwamba anajua ya kuwa Mteteaji wake yu hai na nafsi yake itamwona na macho yake yatamtazama. Baba Mtakatifu mwishoni, anawataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awafundishe kuwa na moyo wa matumaini katika Fumbo la Ufufuko, kwa njia hii wataweza kujifunza kuishi kwa matumaini katika ujio wa Kristo Yesu, utakaowawezesha kukutana na kuonana na ndugu zao waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.