2017-01-30 09:38:00

Msibweteke ukoma bado upo! Kiafya, kiakili, kimaadili na kitamaduni!


Jumuiya ya Kimataifa kamwe isibwete kuhusu ugonjwa wa Ukoma duniani licha ya mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana, kwani Ukoma bado upo. Ombi maalum kwa wadau mbali mbali wenye fursa, uwezo na ujuzi wa kushughulikia ugonjwa wa Ukoma waendelee kufanya kazi kwa bidi, juhudi na maarifa kusudi wahanga wa Ukoma waweze kupata msaada na faraja. Hii ni changamoto kubwa kwa Wakristo kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliwaonea huruma, akawagusa na kuwaponya kutokana na Ukoma.

Wakristo wawe faraja na kimbilio; tayari kuwasaidia, kuwatambua na kuwahangaikia wahanga wote wa ugonjwa wa Ukoma: kwa kuwapatia misaada ya hali na mali; kwa utayari wao; kuwapokea na kuwatembea haki kama inavyostahili kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kuwatenga, kuwabagua au kuwanyanyapaa! Kutekeleza yote haya kwa dhati ni kudumisha utu wa binadamu na hadhi ya Ukristo!

Haya yamesemwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican, katika maadhimisho ya Siku ya 64 ya Mapambano ya Ugonjwa wa Ukoma duniani, yaliyoadhimishwa, hapo tarehe 29 Januari 2017. Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, ugonjwa wa Ukoma tangu zama za kale umekuwa ni wakutisha na kuogopwa sana kutokana na tabia yake ya kumuumiza mwanadamu, kumnyonyoa viungo vyake na hata kumharibia sura yake. Ni ugonjwa unaompotezea mtu amani na utulivu wa ndani pamoja na kumkosesha uwezo wa kujikimu na kujitegemea.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anasema licha ya ugonjwa wa Ukoma unavyofahamika katika afya ya mwanadamu, lakini pia Jamii inachangamotishwa kutambua kwamba, kuna mifumo mbali mbali ya Ukoma inayomtenga mwanadamu na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake. Huu ni Ukoma wa: akili, kimaadili, kitamaduni kwa kukumbatia mno malimwengu, kwa kujikita katika ubinafsi sanjari na kukumbatia utamaduni wa kifo unaodhalilisha Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu. Hii ni changamoto kubwa kwa Jamii kutokana nan a hulya ya watu wa Mungu na Wakristo katika ujumla wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.