2017-01-30 14:34:00

Mashuhuda wa imani wanalitegemeza na kulienzi Kanisa!


Leo hii kuna umati mkubwa wa mashuhuda wa imani wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na kwamba, nguvu ya Kanisa inajidhihirisha kwa namna ya pekee, kutoka kwenye Makanisa yanayoteseka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto na mwaliko wa kuwakumbuka Wakristo wanaoteseka kwa sababu ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwani wao ni chemchemi ya matumaini ya Kanisa la Kristo! Mashujaa hawa wa imani ni wengi kuliko hata ikilinganishwa na wale waliouwawa kwenye Kanisa la mwanzo, lakini kwa bahati mbaya, hawa si sehemu ya habari inayopatiwa kipaumbele cha pekee na vyombo vya mawasiliano ya jamii!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 30 Januari 2017 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kwa kuongozwa na Waraka kwa Waebrania, unaowachangamotisha waamini kufanya kumbu kumbu hai kwa waamini walioshuhudia na kumwilisha fadhila ya imani na unyenyekevu katika maisha yao! Hawa ni ni kama Mzee Abramu, Baba wa imani aliyetoka katika nchi yake na kuelekea katika nchi ya ugenini.

Sura ya kumi na moja ya Waraka kwa Waebrania anasema Baba Mtakatifu inachambua Mashuhuda wa imani waliotendewa makuu na Mwenyezi Mungu. Hawa ni akina Gideoni, Baraka, Samsoni na Yeftha, Daudi na Samweli, bila kusaha Manabii walioshuhudia ukuu na utakatifu wa Mungu katika maisha yao. Kundi la Pili anakaza kusema Baba Mtakatifu ni kumbu kumbu ya Mashuhuda wa imani walioteseka na hatimaye, kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu waliopondwa kwa mawe na kuuwawa kwa ukatili wa upanga.

Ni waamini waliokuwa na dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu, lakini wamekuwa ni mashuhuda wa Kristo kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Hawa ni mihimili na nguzo ya Kanisa na kwamba, leo hii kuna umati mkubwa wa mashuhuda wa imani hata kuliko ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo, lakini hawa si sehemu ya habari zinazopewa kipaumbele cha pekee katika tasnia ya habari. Lakini, wanateswa, wanauwawa na kutupwa gerezani.

Hawa ndio wale wanaoshuhudia utukufu na utakatifu wa Kanisa. Ni mapadre na watawa wanaotumikia vifungo jela miaka nenda miaka rudi; wanafanyishwa kazi za nguvu na wala hakuna anayedai haki zao msingi. Waamini hawa ndio wale waliobahatika kupata mafanikio makubwa katika maisha na utume wao! Ni Makanisa madogo na yenye waamini wachache lakini bado yana nguvu ya ushuhuda kwani damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo wanasema Mababa wa Kanisa. Kanisa bila mashuhuda wa imani, ni sawa na Kanisa bila ya uwepo wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake, kwa kuwataka waamini kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea mashuhuda wa imani, kwani wao ni chemchemi ya nguvu na jeuri ya Kanisa. Ni mashuhuda wa imani wanaoliimarisha Kanisa kwa kujisadaka bila ya kujibakiza; ni mbegu ya Ukristo itakayochipuka na kuzaa matunda kwa wakati wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwakumbuka Wakristo wanaoendelea kuteswa sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kumshukuru Roho Mtakatifu anayeendelea kuwategemeza Wakristo katika shida na magumu yao ya maisha, ili waendelee kumtolea ushuhuda Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.