2017-01-29 14:19:00

Ukoma ni ugonjwa unaoendelea kuwaandama maskini!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 29 Januari 2017, aliwakumbusha waamini kwamba, tarehe 29 Januari 2017, Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya 64 ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukoma Duniani. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani, lakini hata hivyo bado ni ugonjwa ambao unaendelea kuwaandama maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani kuendelea kuwasaidia wagonjwa hawa kwa kuwapatia tiba muafaka sanjari na kuwapatia fursa ya kurejea tena katika maisha ya kijamii. Baba Mtakatifu anawahakikishia wote sala na sadaka yake katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi kuendelea kuonesha uwepo wake wa karibu kiroho kwa wananchi wa Italia walioguswa na kutikiswa na majanga asilia kwa siku za hivi karibuni. Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuonesha moyo wa huruma, upendo na mshikamano. Baba Mtakatifu anasema, kusiwepo na ukiritimba unaokwamisha mchakato wa kuwasaidia wahanga hawa wanaoendelea kuteseka sana.

Mwishoni, Baba Mtakatifu aliyaelekeza mawazo yake kwa bahari ya  chama cha vijana wakatoliki Italia, waliofanya maandamano ya amani, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Kuzungukwa na amani”. Umati huu umeongozwa na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma pamoja na viongozi wa utume wa vijana, wazazi na walezi. Kabla ya kufika uwanjani hapa waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la “Santa Maria in Vallicella”. Watoto hawa walisoma ujumbe wa amani na hatimaye kupeperusha tufe alama ya amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wote amani, unyenyekevu na mshikamano katika familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.