2017-01-29 14:09:00

Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, inatoa nafasi kwa waamini kutafakari Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu katika Agano Jipya. Yesu anawafunulia watu mapenzi ya Mungu kwa kuwaonesha njia inayowapeleka katika furaha, ujumbe ambao tayari ulikuwa umekwisha fumbatwa hata katika vitabu vya Manabii katika Agano la Kale. Kimsingi, Mwenyezi Mungu yuko karibu na maskini na wale wote wanaoteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa, ili kuweza kuwapatia heri na furaha mintarafu utekelezaji wa masharti yake.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 29 Januari 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, furaha hii inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika moyo wa watu wenye umaskini; watu wenye kiu ya haki; na wale wanateseka; mambo ambayo wanapaswa kuyapokea kwa imani kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu. Hii ni hija ya maisha ya kumfuasa Kristo yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani!

Baba Mtakatifu Francisko kwa  namna ya pekee, ameamua kukita tafakari yake kwenye heri ya kwanza inayosema, “Heri maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao”. Maskini wa roho ni watu ambao wamejifunza kuwa wanyenyekevu, wapole na wenye moyo thabiti, watu wasiolalama, bali daima wako wazi kwa neema ya Mungu. Furaha ya maskini wa roho inafumbatwa katika mambo waliyonayo mbele ya Mungu. Ni watu wenye mali za dunia, lakini wamebahatika kuzitumia kadiri ya mpango wa Mungu kwa kushirikiana na wengine sanjari na kuendeleza wema wa Mungu hata katika mambo ya kawaida bila kumezwa na malimwengu.

Furaha ya maskini wa roho ni utenzi wa shukrani na utambuzi wa ukuu wa Mungu kwa neema na baraka zake, kama Baba na Muumbaji, tayari kujiweka wazi mbele ya Mungu kwa kutambua ukuu na wema wake kwa ajili ya ulimwengu licha ya udhaifu na mapungufu ya binadamu! Maskini wa roho ni Mkristo ambaye hajifungamanishi na mambo yake binafsi; utajiri wa mali aliyo nayo, bali ni mwamini anayesikiliza kwa makini, kwa heshima na kujiweka tayari kutekeleza maamuzi yaliyotolewa hata na watu wengine.

Hiki ni kiini cha umoja, upendo na mshikamano ndani ya Jumuiya za Kikristo, kinyume kabisa na kinzani, migawanyiko na mipasuko chungu mbovu! Unyenyekevu na upendo ni tunu muhimu sana katika mafungamano ya maisha ya Kikristo. Maskini wa roho ni vyombo na wajenzi wa ufalme wa Mungu unaojikita katika udugu na mshikamano. Baba Mtakatifu anakazia kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa kuondokana na “roho ya kutu” na badala yake kuwa wazi tayari kutembea katika njia ya upendo. Baba Mtakatifu anahitimisha tafakari yake kwa kusema, Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha maskini wa roho, kwa sababu alijitoa bila ya kujibakiza, akawa mnyenyekevu katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Bikira Maria awasaidie waamini kujisadaka na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma, ili aweze kuwakirimia zawadi, lakini zaidi msamaha wake usiokuwa na kifani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.