2017-01-28 15:02:00

Waamini jengeni utamaduni wa huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamekuwa ni fursa kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi meme kujifunza mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu: kiroho na kimwili! Askofu Olivier Michel Marie Schmitthaeusler wa Jimbo Katoliki la Phnom Penh nchini Cambodia amewaandikia waamini wake Waraka wa Kichungaji unaowataka kujenga, kudumisha na kushuhudia utamaduni wa huruma ya Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku!

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko kati pamoja nao na anajifunua kwa namna ya pekee miongoni mwa wadogo, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hawa ni watu wasiokuwa na makazi maalum, watu ambao wamepokonywa ardhi yao na watu wenye fedha; ni wakimbizi na wahamiaji; ni wanafamilia wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato. Mwenyezi Mungu anaendelea kujifunua hata kwenye familia zinazokabiliana na kinzani na mipasuko ambayo wakati mwingine inasababishwa na ukosefu wa uaminifu, maadili, ukweli na kiasi.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, anajionesha hata miongoni mwa waathirika wa mchezo wa kamali unaowatumbukiza watu katika tamaa ya utajiri wa haraka haraka, lakini matokeo yake, wanajikuta wakiwa wamepigwa “chali miguu juu kama mende” kwa kufilisika kwani wametumia vibaya fedha na rasilimali ya familia kwa mambo ya anasa. Kwa mshangao mkubwa, Mwenyezi Mungu anajionesha miongoni mwa vijana wanaoteseka kwa kutumbukizwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na utumwa mamboleo; vijana wanaotaka kuokolewa na janga hili la maisha, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa maisha yanayosimikwa katika kanuni maadili, ujasiri, matumaini na hali ya mtu kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo yake binafsi pamoja na jamii inayomzunguka!

Askofu Olivier Michel Marie Schmitthaeusler katika Waraka wake wa kichungaji kwa familia ya Mungu Jimboni mwake, anaendelea kutaja litania ya maeneo ambamo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anaendelea kujifunua  na kutembea na watu wake, ili kuwasaidia kuleta mabadiliko, tayari kutembea katika mwanga wa matumaini katika maisha! Anasema, Mwenyezi Mungu anajionesha hata katika maeneo ya kazi, ambamo utu na heshima ya binadamu havipewi kipaumbele cha kwanza na matokeo yake ni viongozi kupenda kuonesha jeuri ya madaraka na fedha ambayo kwa wengi imegeuka kuwa ni sabuni ya roho!

Waraka huu wa kichungaji kwa familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Phnom Penh nchini Cambodia, ni kilele cha hitimisho la maadhimisho ya miaka mitatu ya Injili ya upendo miongoni mwa familia ya Mungu nchini Cambodia sanjari na hitimisho la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, changamoto kwa sasa ni kuendelea kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu nchini Cambodia, ili kuonja uwepo endelevu wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Familia ya Mungu nchini Cambodia inahamasishwa kuhakikisha kwamba, inatambua na hatimaye, kujikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa kwa ajili pamoja na watu wote wa Mungu. Ni fursa ya kujenga utamaduni na madaraja ya kukutana na watu, tayari kusaidiana katika mchakato wa maboresho ya maisha: kiroho na kimwili. Ni wakati wa kuiachia neema ya Mungu kugusa undani wa watu tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha, haki na upendo unaomwilishwa katika haki jamii.

Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini kila mmoja amekirimiwa zawadi na wajibu anaopaswa kuutekeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia nzima ya Mungu nchini Cambodia. Huu ni wakati wa huruma ya Mungu, unaoonesha na kushuhudia uwepo endelevu wa Mungu katika maisha ya watu! Utawala wa mabavu nchini Cambodia umeharibu kwa kiasi kikubwa huduma katika sekta ya elimu, afya, uchumi na maendeleo endelevu! Matokeo yake ni umaskini wa hali na kipato! Leo hii asilimia 60% ya idadi ya wananchi wa Cambodia wana umri chini ya miaka 22!

Ni vijana wa kizazi kipya waliozaliwa na wazazi ambao wamekumbana na utawala wa chuma, kiasi kwamba, hata mchakato wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni ulivurugwa kwa kiasi kikubwa. Hawa ni vijana ambao wamelelewa na kukua kwa kuangalia mifumo ya familia kutoka kwenye televisheni na mitandao ya mawasiliano ya jamii kwa kuona vinaelea na kusahau kwamba, vimeundwa! Hawa ni vijana ambao wanakosa dira na mwelekeo sahihi katika maisha, kwani wanajikuta wakiwa wametumbikia katika ubinafsi, uchu wa mali, fedha na utajiri wa haraka; ulaji wa kupindukia unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwani hapa kinachoheshimiwa si utu wa binadamu, bali mali na vitu alivyo navyo! Waswahili wanasema hapa hapendwi mtu isipokuwa pochi yake! Huo ndio upendo unaojikita katika falsafa ya nipe nikupe na matokeo yake ni kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! Kutokana na changamoto hizi zote, Kanisa linataka kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai, upendo na mshikamano wa dhati; utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza!

Mwishoni, Askofu Olivier Michel Marie Schmitthaeusler anasema, umaskini na mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema ndicho chanzo kikuu cha majanga yanayoendelea kuwakumba wananchi wengi wa Cambodia! Matokeo yake ni kutumbukia katika utumwa wa ulevi wa kupindukia, kinzani na migogoro ya kijamii na kifamilia; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na mchezo wa kamari; mambo ambayo ni kielelezo cha utamaduni wa kifo.

Utamaduni wa huruma ya Mungu unapania kuipatia familia ya Mungu utu na heshima yake, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia na uhai. Kanisa linataka kuwajengea uwezo watu wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kutambua kwamba, kazi ni kielelezo cha utu, heshima na utimilifu wa binadamu! Wazazi na walezi wanawajibika kuwalea na kuwafunda watoto wao tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni na kimaadili, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.