2017-01-26 09:54:00

Liwezesheni Kanisa Tanzania kutangaza na kushuhudia ukweli na maadili


Wito umetolewa kwa Wakurugenzi wa Mawasiliano majimboni na Wakurugenzi wa Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Tanzania kuhakikisha wanaendelea kufanya utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kufuata sheria na taratibu za Nchi huku wakitiwa shime kuzilinda tunu msingi za maisha Kikristo zisitikiswe na sheria mpya ya huduma ya habari ya mwaka 2016. Akizungumza wakati wa kikao cha dharura cha Wakurugenzi wa Mawasiliano majimboni na Wakurugenzi wa Vyombo vya habari vya Kanisa Katoliki nchini, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini, jijini Dar es Salaam, Jumanne tarehe 24 Januari 2017, Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma amewapongeza wanahabari wa Kanisa Katoliki kwa majukumu makubwa na magumu ya Uinjilishaji waliyo nayo.

“Mnaifanya katika “angle” mbalimbali, ninyi ni Wainjilishaji nambari moja na kama ukitaka kuielezea Biblia ama Habari Njema na kuwafikia watu kwa urahisi ni kupitia viganja vyenu, kalamu zenu na karatasi zenu…tunaona watu wana kiu kubwa ya kupata taarifa mbalimbali zinazowazunguka; kupata Habari Njema na mbovu lakini ninyi tukiamini kama waandishi Wakristo Wakatoliki na katika taasisi za kikanisa, tunaamini sehemu kubwa ya mawasiliano yenu mtafikisha Habari Njema inayomhusu mwanadamu na itajengwa, kupambwa na kufinyangwa  kwa tunu msingi za maisha ya kikristo maahali popote,” amesema Askofu Mzonganzila.

“Tunapokuwa tumefika hapa kujadili pia juu ya sheria hii lengo letu ni kuona kwamba tunu msingi za maisha ya Kikristo na kikanisa hazitikiswi na sheria, kumbe, tunashukuru kwa mwaliko huu lakini, ninaamini kwamba akili yote iliyopo hapa wajumbe, mliojikusanya hapa mnaweza kutoa kitu kitakachotusaidia sana …inaweza kuwa na ujenzi mkubwa kiimani kimawasiliano na mahusiano kati yetu sisi wenyewe, na serikali inayotuongoza, kati yetu na waamini na kati yetu na wanachi, huduma yenu siyo ndogo, siyo ya kudharauliwa na inapaswa kupewa uzito wa kipekee… nilipokuwa naongoza idara hii niliona umuhimu na ugumu wake na hasa katika ulimwengu wa mawasiliano na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari!

Wakiati huo huo, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tawi la Dar es Salaam (Msimbazi Centre), Padri Dkt. Charles Kitima amesema sheria mpya ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 iliyosainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli iwajenge kutenda utume wa Uinjilishaji kwa kuzingatia kanuni maadili, nidhamu, uadilifu, ukweli na kuzingatia sheria na kanuni za Nchi. Aidha Dkt. Kitima amewaasa Wakurugenzi na wanahabari wa Kanisa Katoliki nchini  Tanzania kusoma hati maalum ya Inter Mirifica ya mwaka 1965 na Hati za Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican ili walifahamu kwa undani msimamo wa Kanisa Katoliki katika masuala ya sayansi ya mawasiliano ya jamii ili iweze kuwasaidia katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili sanjari na wanahabari walei kupata majiundo endelevu na ya kina katika masuala ya Katekesi na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kutambua na kusimamia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa.

“Pamoja na maelezo mengi kuhusu sheria hii, sisi vyombo vya habari vya Kanisa viendelee kutuweka kuwa makini katika utendaji wetu wa kazi za Uinjilishaji ili tusije kujikuta tumeingia katika matatizo… kweli tunahitaji uhuru wa kujieleza na binadamu wanahitaji uhuru wa kufanya mawasiliano hata sheria za kimataifa tangu kuumbwa kwa ulimwengu zinatambua uhuru wa kupata na kutoa habari,” amesema. Ameonya licha ya kuwepo na tahadhari katika kukiuka sheria lakini Kanisa liepuke woga wa kushindwa kusema na kusimamia ukweli kwa jamii ama kuhubiri Injili, kukemea ikiwemo na kutoa angalizo kwa mafao, ustawi, utu na heshima ya binadamu.

“Mjitahidi kubobea katika taaaluma yenu…pitieni na kutoa ushauri wa kitaaluma kwa wanaosema kwa niaba ya Kanisa, na wenye mamlaka hayo ni Maaskofu, Mapadri, Makatekista na Viongozi wa walei; pitieni ujumbe wanaohitaji kuutoa na kwa Mababa Maaskofu kupitia barua za kichungaji kabla ya kuzitoa ili kuepuka kukiuka sheria…kabla Askofu hajatoa mahubiri tukiacha mahubiri ya kichungaji ni vizuri kujuwa na kumuuliza Baba Askofu mapema kwamba katika tukio linalokuja, Je, analo tamko lolote hili kuepuka kuingia katika mgogoro na serikali,”amefafanua.

Padri Charles Kitima amesema kiimani Viongozi wa Kanisa wanayo mamlaka ya kimaadili na kikanisa ya kuongea na kukemea lakini kwa nyakati za sasa ili kuendana na sheria mpya ya uenezaji wa habari kuna umuhimu mkubwa wa elimu kwa kutoa semina kwa wale wanaoongea kwa niaba ya Kanisa ili waweze kuwa na tahadhari huku akitolea mfano sehemu ya 37 na 38 katika sheria hiyo mpya kuhusu kashfa, kuwa ni Rais pekee na wabunge wakiwa bungeni wanayo kinga ya kashfa,” waepuke kutaja majina ya watu wanapotaka kurekebisha makosa ya watu, mtu ama kikundi fulani na kwamba semina hizo ziandaliwe kitaifa na kimajimbo. “Lakini kipengele hiki kilipaswa kuongezewa ‘nyama’ kuna watu wamepewa haki ya kisheria kutukana kwa mujibu wa sheria… is absolutely priveleged siyo relatively kwa hiyo hata kama limekiuka haki za binadamu ambayo ndiyo kigezo cha sheria za kimataifa wao ni ruksa,” amefafanua Dkt. Kitima.

Amezungumzia suala la wanahabari wa kanisa kujiridhisha kabla ya utoaji wa habari kwa kuwatumia wataalamu wanaohusika na mada husika,kutumia nyaraka kupitia mitandao ili kufikisha ujumbe sahihi lakini pia wanapaswa kuzifuatilia habari mbaya na kuzifikisha katika eneo husika ili kurekebisha badala ya kukimbilia kuandika katika vyombo vya habari kupitia habari za uchunguzi kadiri ya utaalamu wao. Padri Kitima ametaadharisha upokeaji na usambazaji wa taarifa wasizokuwa na uhakika hasa katika makundi ya “Whatsapps” na mitandao mingine ya kijamii,” hasa mapadri na watawa epukeni kupokea na kusambaza taarifa usizokuwa na uhakika na chanzo cha habari ili sheria isije kukubana.”

Awali wakihitimisha mapendekezo yao ambayo yatafikishwa katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ajili mang’amuzi zaidi ,wawakilishi wa vikundi vya washiriki hao, Getruda Madembwe na Padri Sixmund Nyabenda wameelezea umuhimu wa vyombo vya habari vya Kanisa kushikamana na kushirikishana katika utoaji wa habari ikiwemo na kuwahusisha wataalamu wa Kanisa Katoliki waliobobea katika nyanja mbalimbali kupitia tena sheria hiyo kwa faida ya vyombo vya Kanisa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC), Bernard James amewasihi wakurugenzi wa mawasiliano na wakurugenzi wa vyombo vya habari vya kikanisa kuwa na sauti moja hasa kunapotokea matukio ya kitaifa, kushirikiana katika utoaji wa habari na utafutaji wa habari. Bwana Bernad ameshauri kushiriki kwa pamoja Siku ya upashanaji habari inayotarajia kufanyika mwaka huu 2017 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe” Is. 43:5: Kutangaza Matumaini na Kuaminiana katika nyakati zetu” kama ulivyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Januari 2017. Amewasihi kuandika habari zenye utafiti, vyanzo vya uhakika na uchunguzi wa kina; habari zenye ukweli na uwazi ambazo zitawaweka huru na kusisitiza kupitia kabla matamko na jumbe zinazotolewa na Maaskofu kitaaluma ikiwemo na kutoa ushauri ili kuepuka mivutano na serikali.

Ameviagiza vyombo mbalimbali vya habari vya kanisa Katoliki nchini Tanzania kuripoti matukio mbalimbali yanayoendelea kufanyika ikiwemo na miradi inayofanywa na majimbo katika jamii kwa kusaidiana na serikali, lakini zaidi kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kuendelea kutangazwa na kushuhudia na wote kama kielelezo cha imani tendaji!

Na Thompson Mpanji.

Dar es Salaam, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.