2017-01-26 11:56:00

Hofu ya Mungu ni ufupisho makini wa heri za mlimani!


Mtoto mmoja alimuuliza baba yake. “Baba, hivi Mungu ni mkubwa kiasi gani?” Baba yake akatazama juu angani akaona ndege ya abiria akamuuliza mwanae “mwanangu, ile ndege ina ukubwa Gani?” Mtoto akajibu ni ndogo sana. Basi Baba yake akamchukua hadi uwanja wa ndege walipofika karibu na ndege akamuonesha ndege akamuuliza  “ile ndege ina ukubwa gani?” Mtoto akajibu “Hiyo Ndege ni Kuuuubwa sana” basi Baba yake akamwambia  ... “Mwanangu, hivyo ndivyo ilivyo kuhusu ukubwa wa Mungu, mara zote hutegemea wewe upo umbali gani ili kuona ama kujua ukubwa wake. Ukiwa mbali na Mungu kiroho utaona Mungu ni mdogo sana, ila ukiwa karibu naye wakati wote utamwona ni mkubwa kuliko kawaida na hakuna mfano wa kulinganisha”.

Masomo ya Dominika hii yanatuweka katika uchaguzi wa maisha; kuwa upande wa Mwenyezi Mungu ili kupata heri au kuwa kinyume naye na kuangamia. Hii yote inawezeshwa na ukaribu wetu kwake. Tunapokuwa naye na kuwa na hofu naye tutautambua ukubwa wake na hivyo tutajinyenyekeza na kuyatimiza mapenzi yake hapa duniani. Kwa upande wa pili tunapomweka mbali nasi basi hatakuwa na nafasi moyoni mwetu na hivyo kumdogosha zaidi huku sisi tukiendelea kujikuza. Mtume Paulo anauhitimisha waraka wake wa kwanza kwa Wakorinto akisema: “Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana”. Tukiyatafakari maisha yetu leo hii tunagundua kwamba ipo kazi ya kufanya. Kazi hiyo kwetu sisi Wakristo ni kumtafuta Bwana na kuyatimiza yale anayotuagiza. Tukizidi kumweka mbali tutasahawishika kumwona yu mdogo na matokeo yake kumdharau na hata kumpuuzia mbali kabisa.

Somo la kwanza limetuwekea fadhila ya unyenyekevu kama nyenzo muhimu ya kumkaribia zaidi Mungu na kuutambua ukuu wake. Hofu ya Mungu huchagizwa na unyenyekevu. Nabii Safania anatualika akisema: “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake ... huenda mkafichwa siku ya hasira ya Bwana”. Huu ni mwito wa kumkaribia Mungu. Ni tangazo la ujio wa hasira ya Mungu ambayo kuponywa kwake ni kwa njia ya kumkaribia Yeye tu. Lakini Mungu anajifunua kwetu katika maisha ya kawaida ya kila siku, anajifunua katika jamii yetu tunayoishi. Mwaliko huu wa kumkaribia ni maelekezo kwetu kuangalia udugu wetu wa kikristo; ni namna gani ninaishi na mwenzangu aliyeumbwa na Mungu na aliye sura na mfano wa Mungu kama mimi.

Heri nane tunazopewa katika somo la Injili ni dira kwetu na tutakapofanikiwa kuzitekeleza tutauona ukuu wa Mungu na kumwabudu katika kweli. Heri hizi zinajifunua katika sehemu ya mwisho ya utabiri wa Nabii Sefania anaposema: “nitasaza ndani yako watu walioonewa, nao watalitumainia jina la Bwana ... hawatatenda uovu wala kusema uongo; ulimi wa adaa hautaonekana kinywani mwao ... wala hapana mtu atakayewaogofya”. Ni vema kuzitafakari heri hizi kwa pamoja na kung’amua ulazima wake kama mwongozo wa maisha yetu ya kikristo.

Umaskini wa roho hutuchagiza kujisikia hatuna kitu mbele zake na hivyo kuchuchumilia daima kujazwa na uwepo wa utukufu wake. Umaskini huu haurandanishwi na ufukara wa mali za kidunia au mamlaka na makuu ya ulimwengu, bali ni ile hali ya ndani ya kujisikia mtupu (anawim), kujisikia unayehitaji kujazwa daima neema na baraka za Mungu. Kujiona si lolote kama uwepo wako katika jamii ya wanadamu haujazwi na uwepo wa Mungu na kumfunua Mungu. Mtakatifu Yohane wa Msalaba anauzungumzia umaskini wa roho akisema kwamba: “Yeye aliye maskini wa roho hushibishwa kwa kuwa na furaha zaidi kwa sababu atapaswa kuyaunda yote katika hali ya kutokuwa na chochote na hivyo kuutunza uhuru wa kiroho katika kila kitu”.

Walio na huzuni wanazungumziwa na Mwinjili Mathayo ni wale wanaoumia, wale wanaokosa raha kwa sababu ya kupindishwa kwa amri za Mungu na hivyo uovu kutawala katika jamii. Upole humfanya mmoja kuwa mkarimu na tayari kuwapatia wengine nafasi. Wenye rehema hujifunua katika sura nyingi. Kwanza tunawaona katika wale wanaotoa msamaha kwa wengine. Hili ni dai la kututaka kutafuta upatanishi na wengine na kuonesha upendo hata kwa adui (Mt 5:44 – 47). Hapa tunaona muunganiko na heri ile wanaopewa wapatanishi. Tendo hili pia ni tendo la ukarimu na hivyo huchagizwa na upole wetu na mwishoni hujenga amani. Wenye rehema pia huonekana katika matendo ya huruma hasa kwa wahitaji. Hawa ni wale ambao tulihimizwa sana kujifunua kwao wakati wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, yaani, walio uchi, walio vifungoni, wenye njaa, wenye kiu, walio wagonjwa, wageni au wakimbizi (Mt 25:31 – 46).

Usafi wa moyo huelezea usafi wa kimaadili na kiutu. Zaburi ya 24 inamtaja mwenye mikono safi na moyo mweupe, yeye ambaye anastahili kuupanda mlima wa Bwana, kuwa ni “yeye asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, na wala kuapa kwa hila”.  Hii inadokeza uaminifu katika amri za Mungu  na kuabudu kweli  kinyume na unafiki katika maisha. Na heri ya mwisho inatuelekeza katika kumshuhudia Kristo aliye haki na ukweli. Ni dai la kutuita kupokea wito wetu katika hali zote kwa haki na ukweli bila kupindisha hata kama inatudai kutoa sadaka. Heri hii inadokeza sadaka ya Kristo Msalabani, sadaka ambayo inafumbata fumbo zima la ukombozi na kuelezea maana halisi ya hofu ya Mungu, yaani kutii amri zake na kuyatimiza mapenzi yake.

 Heri zote hizi zinatukusanya katika kumweka Mungu kama kipaumbele na dira ya yote. Hii inatufanya sote kujiona tu wamoja na asili yetu kuwa ni moja. Inatufanya kuhangaikia wokovu wa wote, ustawi wa wote; inatufanya kuiona sura ya Mungu iliyoumbika ndani ya kila mmoja. Hivyo heri nane ni katiba ya maisha ya mkristo na nyenzo ya kuufanya hai utume wa Kristo katika jamii ya wanadamu. Maisha yetu yanapotutenga na wenzetu taratibu yanaanza kututenga na Mungu. Yeye ambaye anashindwa kujitwika heri anazotupatia Kristo ni aghalabu kumwona mwenzake katika jamii na hivyo hawezi kuustawisha ujumbe wa Injili ya Kristo unaojikita katika ukombozi wa mwanadamu mzima. Fadhila ya unyenyekevu, kama ulivyo mwaliko wa Nabii Sefania ni msaada kwetu. Unyenyekevu unatusaidia kujifunua, kujitafakari na kuitambua nafasi yetu mbele za Mungu na mbele za wenzetu na hivyo kutoa nafasi kwa wengine na hata kunuia wapate fanaka daima. Tuliombe paji hilo la unyenyekevu na tujiepushe na kiburi ambacho hutuweka mbali zaidi na Mungu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.