2017-01-25 10:27:00

Ni patashika nguo kuchanika kwa vijana mwaka 2019 huko Panama


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Hii ni hija ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaodhaminishwa na Mama Kanisa katika tunza na ulinzi wa Bikira Maria, ili kweli waweze kumjifunza Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria aliyesikiliza kwa makini na kutenda yote kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha yake!

Kardinali Kevin Farrel, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yataongozwa kwa Ibada kwa Bikira Maria, ili kukazia umuhimu na nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya. Itakumbukwa kwamba, waamini wengi wa Amerika ya Kusini wana Ibada kwa Bikira Maria.

Kardinali Farrel tayari amekwisha tinga nchini Panama ili kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Panama kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani; kwa kushirikiana kwa karibu sana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi, kwani liliunga mkono Panama kuwa ni mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Panama ina umuhimu wa pekee katika mchakato wa Uinjilishaji Amerika ya Kusini, kwani kutoka Panama, cheche za Habari Njema ya Wokovu ziliweza kuenea sehemu mbali mbali za Amerika ya Kusini. Kunako mwaka 1513 Jimbo la Antiqua, huko Panama likaundwa. Hili ni Jimbo la kwanza kabisa kuundwa Amerika ya Kusini.

Kardinali Farrel anakaza kusema si haba kwamba, Panama imepewa upendeleo wa pekee ili kuwa ni mwenyeji wa Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 kwani inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuwahudumia na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji  kutoka sehemu mbali mbali za Amerika ya Kusini. Wakati huu ambapo Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutafakari kuhusu kile kinachoitwa “kero” ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, nchini Panama, itakuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana: sababu, maana na mchango wa wakimbizi na wahamiaji katika ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu kwa watu wa nyakati hizi.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 itakuwa ni fursa nyingine tena ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: ushuhuda wa imani kiasi hata cha Wakristo kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; ushuhuda wa maisha ya kiroho na sala; ushuhuda unaojikita katika tafakari ya Neno la Mungu na Sala kwa ajili ya umoja na mshikamano wa Wakristo. Hizi pia ni jitihada za kujenga na kudumisha uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa nafasi hii, hawa ni wakimbizi na wahamiaji huko Amerika ya Kusini.

Kardinali Kevin Farrel, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema tarehe 22 – 27 Januari 2019 ni kipindi ambacho kinakabiliwa na changamoto nyingi kwa upande wa vijana walioko shuleni na vyuo vikuu. Huu ni muda wa mitihani kwa wanafunzi sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, ikumbukwe kwamba, si mara ya kwanza kwamba, Siku ya Vijana Duniani inaadhimishwa wakati wa Mwezi Januari, kwani kunako mwaka 1995, Mtakatifu Yohane Paulo II alizungukwa na bahari ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kuadhimisha na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mwezi Januari umechaguliwa kwani ni kipindi muafaka ukizingatia hali ya hewa.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta kutoka Jimbo kuu la Panama anakaza kusema, taarehe 22 hadi 27 Januari ni kipindi kizuri kinachoweza kutoa nafasi kwa vijana kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kwa raha zao wenyewe! Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakumbushwa kwamba wao ndio wahusika wakuu wa maadhimisho haya na kamwe wasiwe ni watazamaji, bali washuke huko mitini, tayari kushirikisha karama, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha, kwani Kanisa linataka kuwasikiliza na kuwapatia majibu muafaka mintarafu mwanga wa Injili. Yaani, Kanisa linawasubiri vijana kwa mikono miwili huko Panama ili kushirikishana tone la imani na kujisikia kuwa kweli ni wadau na wala si watazamaji au watu wa kuja katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.