2017-01-24 14:44:00

Waandishi wa habari: wajenzi wa jamii, mafao ya wengi na wapatanishi!


Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican, katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko wa Sale, Askofu, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa waandishi wa habari Wakatoliki, Jumanne, tarehe 24 Januari 2017, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaombea waandishi wa habari sehemu mbali mbali za dunia, ili waweze kutekeleza dhamana hii nyeti. Watambue kwamba, wao ni vyombo vya ujenzi wa jamii, mafao ya wengi na chachu ya upatanisho na kamwe, wasiwe ni sababu ya utengano wa kijamii, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana!

Katika mahubiri yake, Monsinyo Viganò amewakumbusha wafanyakazi wa Sektretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican waliohudhuria kwa wingi kwenye Kikanisa cha Kupashwa Habari Bikira Maria, kilichoko kwenye Jengo la Mawasiliano, Radio Vatican kwamba, Kristo Yesu ni Kuhani mkuu aliyejisadaka ili kuondoa dhambi za ulimwengu! Kumbe, kwa wale waliopewa dhamana ya mawasiliano ndani ya Kanisa wanapaswa kuwa wazi wanapofafanua mafundisho tanzu ya imani ya Kanisa!

Mtakatifu Francisko wa Sale katika maisha na utume wake alikutana na changamoto za maisha, akasimama kidete katika mageuzi yaliyokuwa yanamzunguka kwa kujikita katika hekima ya mawasiliano bila kuonesha kinzani, mfano bora wa kuigwa. Akajielekeza zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu katika uhalisia wa maisha ya kawaida; akafafanua Mafumbo ya Kanisa na kweli za imani katika lugha iliyokuwa inaeleweka kwa wengi, kielelezo makini cha uwezo wake wa kuwasiliana na watu. Kama Askofu wa Geneva, Uswiss, aliwataka Mapadre na Makatekista wake kuivalia njuga changamoto hii, ili kufikisha kweli za imani katika lugha inayoeleweka na wengi!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau katika tasnia ya habari kuhakikisha kwamba, wanajenga mawasiliano na watu wote bila ubaguzi, kwani lugha ya Kanisa ni kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaowakirimia watu utimilifu wa maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyetumwa na Baba wa mbinguni. Watu wote waonje joto la upendo unaobubujika kutoka kwa Mama Kanisa ili kweli Kristo aweze kufahamika, kupendwa na kutumikiwa. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa njia ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za imani.

Wadau wa tasnia ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa wanakumbushwa kwamba, wao si wamiliki wa Habari Njema, bali ni vyombo vinavyopaswa kutangaza na kushuhudia haki na kweli; furaha, imani na matumaini. Ili kutekeleza vyema dhamana hii, Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau wa vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kufahamu asili na dhamana ya Kanisa katika mchakato wa maisha na utume wake duniani na kwamba, Kanisa linatambua na kuthamini mchango unaotolewa na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kumbe, wafanyakazi katika sekta ya upashanaji habari wanapaswa kunolewa barabara, kuwa na weledi, nidhamu, uwajibikaji tayari kutangaza na kushuhudia: ukweli, wema na uzuri wa Mama Kanisa, tunu ambazo zinapaswa kumwilishwa na mfanyakazi katika vyombo vya habari vya Kanisa ambao wanaalikwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, wema na uzuri na wala si kujitangaza na kujishuhudia wao wenyewe!

Monsinyo Viganò akifanya rejea kwenye Injili ya siku, amewataka wale wote wanaotaka kuwa ni wafuasi wa Kristo kutoka katika ubinafsi wao na kumwendea Kristo Yesu huko aliko, hali inayohitaji toba na wongofu wa ndani ili kujenga mahusiano na mawasiliano. Hii ni dhamana pevu na nyeti katika maisha, inayohitaji ujasiri, ili kuwa kweli ni sehemu ya familia ya Yesu inayomsikiliza na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Waandishi wa habari wanapaswa kupenda, kushuhudia na kutangaza ukweli kwa njia ya maisha na kazi zao kwa jamii. Hapa haijalishi kwamba, wewe ni mwamini au la, bali jambo la msingi ni kwa mwandishi wa habari kuwa mwaminifu kwake binafsi pamoja na jirani zake, daima akitafuta na kudumisha ukweli anaotaka kuutangaza na kuushuhudia. Hii ni dhamana nyeti na pevu anakaza kusema, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican kwamba, waandishi wa habari wajitahidi daima kuutafuta ukweli na kuutangaza na kamwe wasisutwe na dhamiri fuatizi kwa kushindwa kutangaza na kushuhudia ukweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.