2017-01-23 14:29:00

Jifunzeni kutenda katika ukweli, uwazi na utakatifu wa maisha!


Wajumbe wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kitume, “Rota Romana”, Jumamosi tarehe 21 Januari 2016 walizindua maadhimisho ya Mwaka wa shughuli za Mahakama ya Rufaa ya Kitume kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko aliyekazia umuhimu wa majiundo makini na endelevu kwa wanandoa watarajiwa ili kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha vyema Sakramenti ya Ndoa, tayari kuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika Injili ya familia, kitalu cha upendo wa dhati kati ya bwana na bibi kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu!

Tukio hili lilitanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican aliyewataka wajumbe wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kitume kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu jinsi alivyotekeleza dhamana na utume wake katika kazi ya Ukombozi kwa kuwasikiliza watu kwa makini; kwa kuwaponya wagonjwa; kwa kuwaondolea watu dhambi zao pamoja na kuwapatia mahitaji msingi, ili kukuza na kudumisha utu na heshima yao kama watoto wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakakombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu.

Askofu mkuu Becciu anakaza kusema, Yesu alijitahidi katika maisha yake kutekeleza dhamana na utume wake kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kudhani kwamba, alikuwa “amechangnyikiwa”, lakini si kweli, alikuwa akiongozwa na Roho Mtakatifu, ili kujitoa na kujisadaka kama Mwana Kondoo wa Mungu asiye kuwa na mawaa! Kristo alimwaga Damu yake Azizi kama sadaka safi inayompendeza Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za ulimwengu. Wafanyakazi katika Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kitume, wanayo dhamana kubwa mbele yao kwa kutambua kwamba, kuna watu ambao wanakosa usingizi; wanatafuta watu makini wa kuweza kuwasikiliza na kuwapatia majibu muafaka kutokana na matatizo, changamoto na madonda yanayoendelea kuvuja damu katika maisha yao ya ndoa na familia. Ni watu wanaonja chachu ya kushindwa katika maisha, hali inayowasababishia machungu katika nyoyo zao.

Kumbe, wafanyakazi hawa wanatakiwa kuiga mfano wa Kristo aliyejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia watu Injili ya matumaini na upendo na wanapaswa kutambua kuwa, kila karatasi wanayoiangalia na kuipembua ili kuifanyia kazi, nyuma yake kuna sura za watu wanaoteseka na kuhangaika katika maisha ya ndoa na familia; kuna watu wenye madonda makubwa yanayohitaji kugangwa na kuponywa kwa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa njiaya Kanisa lake; ni watu wenye matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya! Jambo la msingi kwa wao ni kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu hawa kadiri ya changamoto inayotolewa na Kristo Yesu, kama walivyofanya pia akina Mtakatifu Agnesi, Bikira na Shahidi.

Yesu ni Mwana Kondoo wa Mungu anayejitwika na kuondoa dhambi za ulimwengu, changamoto na mwaliko kwa wafanyakazi katika Mahakama ya Rufaa ya Kitume kuwa waaminifu kwa Kristo, Injili na Kanisa lake, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa wale wote wenye shida na mahangaiko mbali mbali, wanaohitaji msaada wa kisheria kutoka kwao. Dhamana hii ni nyeti lakini inafumbatwa katika “Huruma ya Kiinjili” na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Kwa hivyo, sheria, kanuni na taratibu zote za Kimahakama zinapaswa kupata chimbuko lake katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Hii ni changamoto ya kutoka katika ubinafsi na kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda na kuwaongoza katika maisha na utume wao, ili kusaidia mchakato wa kueneza upendo na huruma ya Kristo duniani. Huduma hii ya Kimahakama inayotekelezwa kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro inawataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti, tafakari na huduma makini inayotekelezwa kwa moyo wa huruma na mapendo. Wanandoa wenye shida na mahangaiko mbali mbali wanasubiri kutoka Kanisani majibu ya ukweli yanayofumbatwa katika haki na huruma. Mwishoni, Askofu Mkuu Angelo Becciu amewatakia heri na baraka katika maisha na utume wa, ili Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza daima katika upendo, ili kujenga Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa! Utume huu unaweza kutekelezwa kwa kufungamanisha haki na huruma; katika ukweli, uzuri na utakatifu wa familia ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.