2017-01-21 14:54:00

Papa: Wafungwa msizimishe taa ya matumaini ndani mwenu!


Uzima wa binadamu ni kitu kitakatifu kwa sababu tangu mwanzo wake unahusiana na tendo la Mungu la uumbaji na daima unabaki na uhusiano wa pekee na Muumba aliye peke yake kikomo chake. Mungu peke yake ndiye mwanzo wa uhai, tangu mwanzo wake hadi mwisho wake. Hakuna mazingira yoyote yanayoweza kujitwalia haki ya kuharibu moja kwa moja maisha ya binadamu asiye kuwa na hatia. Kwa maneno machache, Kanisa linasema, adhabu ya kifo imepitwa na wakati kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tarehe 17 Januari 2017 amemwandikia barua Padre Marco Pozza, Mhudumu wa maisha ya kiroho kwenye Gereza la “Due Pallazi”, lililoko Padua akimtia shime kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo wakati wa kongamano lililokuwa linajadili kuhusu “Adhabu ya kifungo cha Maisha sanjari na Adhabu ya Kifo” na kwamba, alipenda pia kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wafungwa magerezani kwa njia ya sala na sadaka yake na kwamba, anapenda kukutana nao uso kwa uso, ili kuwapatia tena nafasi ya kuchunguza dhamiri zao, ili kamwe wasijikatie tamaa na kuzimisha moto wa matumaini ndani mwao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuendelea kuwasha moto wa matumaini ni dhamana ya Kanisa na wale wote wanaotoa huduma kwa wafungwa na mahabusu. Utu na heshima yao vinapaswa kuwa ni dira na mwongozo katika utekelezaji wa sheria, taratibu na kanuni za magereza. Baba Mtakatifu anawataka washiriki wa semina hii kuhakikisha kwamba, wanachia ili kuendelea kuwasha mshumaa wa matumaini, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kila mmoja wao!

Hapa, wongofu wa kitamaduni unahitajika ili kutambua kwamba, adhabu ya kifungo jela haina neno la mwisho kwa kuendekeza haki inayoadhibu wala kuridhika na haki malipo ya hasara! Kinachotakiwa hapa ni haki inayopatanisha na kumwezesha mfungwa anapomaliza adhabu yake aweze kuingia tena katika maisha ya kijamii akiwa ni mwema zaidi kuliko alipoingia gerezani. Kifungo cha maisha kisiwe ni suluhu ya matatizo ya kijamii, bali chachu ya kutatua changamoto za kijamii, tayari kutoa nafasi kwa utu na heshima ya binadamu kuanza upya kwa kujiaminisha katika nguvu ya msamaha. Mbele ya Mwenyezi Mungu, anasema Baba Mtakatifu daima kuna nafasi ya kuanza upya, kufarijika na kurekebishwa na huruma inayosamehe. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anaweka safari ya wafungwa wote chini ya huruma na upendo wa Mungu ili kamwe mshumaa wa matumaini ya maisha usizimike!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.