2017-01-21 14:24:00

Papa: Jengeni familia yenye upendo wa dhati kati ya bwana na bibi!


Baba Mtakatifu Francisko amewataka wafanyakazi katika Mahakama kuu ya Rufaa ya Kitume “Rota Romana” kutekeleza dhamana na wajibu wao katika hali ya utulivu, ari, moyo mkuu na upendo kwa Kristo na Kanisa lake, wanapouanza Mwaka wa shughuli za Mahakama, kwa kutambua kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya imani na ndoa takatifu! Pale binadamu anapokengeuka na kumezwa mno na malimwengu anasema Mtakatifu Yohane Paulo II hapo pia ndoa na maisha yako mashakani na hatarini sana kwa kushindwa kujikita katika mambo msingi ya maisha. Waamini wanapaswa kukuza na kudumisha imani itakayowasaidia kuwa na mwelekeo sahihi wa maisha wanapokabiliana na changamoto na magumu ya maisha kwa kutambua kwamba, kweli Mungu yupo!

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika hotuba yake ya mwisho kwa wajumbe wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kitume, aliwataka wajumbe hawa kujiweka wazi mbele ya ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu, ili kufahamu mambo msingi yanayofumbatwa katika maisha ya watu; ukweli wa watu wa Mungu wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu katika Sakramenti ya Ubatizo na kwamba, ukanimungu unahatarisha mafungamano ya mahusiano ya kibinadamu bila kusahau maisha ya ndoa. Kumbe, kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu upendo na ukweli kwani upendo unahitaji kufumbatwa katika ukweli, ili kuwa na ukomavu pamoja na udumifu, ili hatimaye, kushikamana katika hija ya pamoja!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 21 Januari 2017 alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Kitume, “Rota Romana” wakati wa kufungua Mwaka wa shughuli za Mahakama. Ili kweli upendo uweze kuwa thabiti hauna budi kujikita katika ukweli, kwani upendo wa dhati unaunganisha mambo msingi katika maisha ya binadamu na kuwa ni mwanga wa ukuu na utimilifu wa maisha. Bila ukweli, upendo utayumba sana na kuwatumbukiza watu katika ubinafsi, upweke na utumwa kiasi hata cha kushindwa kujenga maisha na kuzaa matunda yanayokusudiwa!

Katika ulimwengu mamboleo kuna tabia ya kutaka kuficha njia za kufikia ukweli wa milele, tabia ambayo hata Wakristo wenyewe wanajikuta wakiwa wametumbukia huko, kiasi cha imani kudhoofika kwa kukosa vigezo asilia katika kutafsiri na kutenda kama mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Haya ni mazingira ambamo kunakosekana tunu msingi za maisha ya kiroho na kiimani kiasi hata cha kuathiri ueelewa wa maisha ya ndoa. Mang’amuzi ya imani kwa Wakristo wanaotaka kufunga Ndoa Kanisani anasema Baba Mtakatifu Francisko yanatofautiana sana.

Kuna baadhi yao ni waamini moto moto katika maisha na utume wa Kanisa Parokiani; baadhi yao, hii inakuwa ni nafasi ya kuingia Kanisani kwa mara ya kwanza; wengine wana maisha yanayofumbatwa katika sala na wengine ni wale wenye uelewa wa juu juu tu kuhusu dini na hata wakati mwingine ni watu ambao wamepoteza imani au hawana hata chembe ya imani katika maisha yao! Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, jambo la kwanza ni majiundo makini na endelevu ya wanandoa watarajiwa ili kuweza kugundua maana ya Ndoa na Familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Wanandoa watarajiwa wasaidiwe kuonja ndani mwao neema, uzuri na furaha ya upendo wa kweli, uliookolewa na kukombolewa na Kristo Yesu. Jumuiya ya waamini inapaswa pia kuwa ni shuhuda wa Injili ya familia, ili kweli wanandoa watarajiwa waweze kuonja uzuri, utakatifu na upendo katika maisha ya ndoa ambayo ni Sakramenti, alama wazi na makini kwa ajili ya wokovu! Kwa njia hii, utume unaookoa kutoka kwa Kristo Yesu, unaweza kuwafikia watu katika uhalisia wa maisha yao ya upendo na hivyo kugeuka kuwa ni utume usiokuwa wa kawaida kwa Jumuiya. Hii ni dhamana ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Kwa baadhi ya vijana Sakramenti ya Ndoa, inakuwa ni fursa ya kupyaisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kufanya mageuzi katika mfumo wa maisha yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii inaweza kuwa ni nafasi muhimu sana kwa vijana kupyaisha mahusiano yao na Kristo Yesu; Habari Njema ya Wokovu pamoja na Mafundisho tanzu ya Kanisa. Kumbe, mihimili ya Uinjilishaji haina budi kuwa makini sana katika maandalizi kwa wanandoa watarajiwa, ili kuwasaidia kuweza kuingia taratibu katika Fumbo la Kristo na Kanisa kwa ajili ya Kanisa.

Huu ni mchakato wa maendeleo ya ukomavu wa imani kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kumfuasa Kristo kwa ari na moyo mkuu. Lengo kwa wanandoa watarajiwa ni kufahamu Sakramenti ya Ndoa wanayotarajia kuiadhimisha ili iweze kuwa halali, haki kisheria na yenye kuzaa matunda mengi kwani maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa ni sehemu ya mchakato wa hija yao ya imani. Ili kufikia hapa, anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kuwa na mihimili maalum ya Uinjilishaji iliyoandaliwa, ikafundwa na kufundika barabara, tayari kutekeleza huduma hii makini kwa ushirikiano kati ya Wakleri na Wanandoa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ari na moyo huu unahitaji “Ukatekumeni mpya” katika matayarisho ya wanandoa watarajiwa, kwani kama ilivyo Ubatizo kwa watu wazima, Ukatekumeni huu ni sehemu ya maandalizi ya kupokea pia Sakramenti ya Ndoa ili kuondokana na shida ya kulazimika kutengua ndoa zenye hitilafu. Pili wanandoa wapya wasaidiwe kuendelea kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa hata baada ya kufunga ndoa Kanisani pamoja na kuwapatia majiundo endelevu, ili kuwa na mang’amuzi mapana juu ya Sakramenti ya Ndoa kwa kutambua na kukuza mambo msingi katika maisha yao ya kifamilia yanayojikita katika upendo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwani Mwenyezi Mungu ni mwaminifu daima.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Jumuiya ya Kikristo inaalikwa kuwapokea, kuwasindikiza pamoja na kuwasaidia wanandoa wapya kwa kuwapatia nyenzo msingi katika maisha yao; kwa kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu; Kwa kukuza na kuboresha maisha yao ya kiroho mintarafu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji Parokiani. Wanandoa wanapobahatika kupata zawadi ya mtoto, Kanisa linapaswa kuwa karibu sana nao, ili kuwasaidia kulea kwani wazazi na walezi wanakumbushwa kwamba wao ni mashuhuda na vyombo vya zawadi ya imani. Wanandoa wapya washirikishwe kwenye vyama vya kitume, ili kuwawezesha kupata majiundo endelevu: Kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu; Maisha ya Sala na upendo wa kidugu!.

Baba Mtakatifu anasema huu ndio ushauri wake wa kitume na kichungaji kwa ajili ya maadhimisho na maisha ya Ndoa. Maparoko watambue dhamana nyeti iliyoko mbele yao ya kuwaandaa wanandoa watarajiwa, ili kuwawezesha kumwilisha kikamilifu upendo na imani; kwa kukazia majiundo awali na endelevu yanayowawezesha kutambua upendo na imani iliyoinuliwa na Kristo Yesu katika Sakramenti ya Ndoa. Utume huu unahitaji ushirikiano wa dhati kati ya Wakleri na wanandoa ili kujenga jamii na familia ambamo kweli bwana na bibi wanashibana kweli kweli. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea kwa Roho Mtakatifu ili awasaidie waamini wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa ndoa na familia, ili kuwasaidia wanandoa kuendelea kuwa na ujasiri wa kuendeleza uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia licha ya changmoto na matatizo yanayoendelea kusababishwa na utamaduni mamboleo usiokuwa na mizizi katika maisha ya watu! Vijana wanapaswa kuwa na ujasiri wa kuamua kuoana, kumbe, Kanisa linapaswa kuwa karibu sana na vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.