2017-01-21 08:40:00

Majibu mepesi mepesi ya wanasiasa kwa kero za wananchi ni kashfa kubwa


Christine Lagarde, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, akichangia mada kwenye maadhimisho ya 47 ya Jukwaa la Uchumi Duniani lililofunguliwa rasmi hapo tarehe 17 Januari na kuhitimishwa tarehe 20 Januari 2017 amewataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati na sera makini za uchumi zitakazosaidia kusongesha mbele libeneke la uchumi duniani, vingimevyo, kinzani na mipasuko ya kijamii itaendelea kushamiri kila kukicha!

Matokeo ya uchumi usiotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu ni kinzani na mipasuko ya kijamii inayojionesha huko Barani Ulaya na Amerika kwani kwa jeshi kubwa la vijana wa kizazi kipya halina fursa za ajira na matokeo yake ni vijana kujikatia tamaa ya maisha. Jambo la pili ni kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na mgawanyo bora zaidi wa rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Hii ni changamoto kwa wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanatoa majibu muafaka kwa changamoto za kiuchumi zinazoendelea kujitokeza na kusababisha mpasuko wa mafungamano ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia.

Majibu mepesi mepesi ya wanasiasa wengi kuhusu kero na hali ngumu ya maisha yanaendelea kuleta kero kubwa kwa wapiga kura wao, kiasi hata cha kujutia ni kwanini waliwachagua viongozi kama hawa wasiothubutu kuona, kusikia wala kuguswa na mahangaiko ya wapiga kura wao! Watu wengi wamekata tamaa ya kupata fursa za ajira kutokana na madhara ya myumbo wa uchumi kimataifa hali ambayo inahatarisha pia ustawi na maendeleo ya watu wengi duniani.

Kuna haja kwa wanasiasa kuwa na sera na mikakati makini ya kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kutambua kwamba, utandawazi ni mchakato usiokwepeka hata kidogo kama alivyokaza kusema Rais Xi Jin Ping wa China wakati alipokuwa anatoa hotuba yake kwenye Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos, Uswiss. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, uchumi wa kimataifa unakua na kuongezeka katika usawa, changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pamoja Serikali ya Marekani; mataifa makubwa yanayoshikilia na kuongoza uchumi ya Jumuiya ya Kimataifa. Sera zinazojikita katika woga na wasi wasi zimepitwa na wakati kwani hiki ni chanzo kikuu cha mipasuko na kinzani za kijamii. Kumbe, ulinzi na usalama vinapaswa kuimarisha na kudumishwa kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.