2017-01-20 16:08:00

Wajumbe wa Vatican na Israeli kukutana tena Machi 2017


Tume ya Kazi ya kudumu kati ya Vatican na Israeli hivi karibuni ilikutana mjini Yerusalemu katika mkutano wa kazi kuhusu majadiliano baina ya pande hizi mbili mintarafu Hati ya Makubaliano Msingi kati ya Vatican na Israeli ya Mwaka 1993, Ibara 10 kipengele namba 2. Bwana Tzachi Hanegbi, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda aliongoza ujumbe wa Israeli na Monsinyo Antoine Camilleri aliongoza ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu.

Wajumbe wa mkutano huu, kwa pamoja wamepongeza hatua ambayo imefikiwa kati ya Israel na Vatican katika mkutano wa kazi na kwamba, wana matumaini kuwa kazi hii itaendelea kufanyiwa tafakari na kuendelezwa zaidi. Mkutano umekiri na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na Waziri wa Haki nchini Israeli kwa kutekeleza kwa kina na mapana Makubaliano ya Pamoja ya Mwaka 1997 juu ya  watu wenye Hadhi Kisheria.

Pande hizi mbili zimekubaliana kuhusu hatua msingi zinazopaswa kutekelezwa kwa ajili ya mkutano utakaofanyika kunako mwezi Machi 2017 mjini Vatican. Baada ya mkutano wa kazi, Kamati ya kudumu, wajumbe wa Vatican na Israeli walifanya kikao cha ushauri kwenye Makao makuu ya Wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Israeli. Wajumbe wamejadili masuala yanayozigusa pande hizi mbili pamoja na kubainisha maeneo ya ushirikiano kati ya Israeli na Vatican kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.