2017-01-20 10:39:00

Papa Francisko anakazia diplomasia na ushirikiano wa kimataifa!


Vatican itaendelea kuimarisha ushiriki wake katika masuala ya kimataifa kwa njia ya diplomasia, ili kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wote. Mpasuko wa Jumuiya ya Ulaya na madhara yake; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani pamoja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti utengenezaji, utumiaji na ulimbikizaji wa silaha za kinyuklia, ni kati ya mchango mkubwa uliotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 19 Januari 2017 huko Davos, Uswiss wakati wa maadhimisho ya 47 ya Jukwaa la Uchumi Duniani lililofunguliwa rasmi hapo tarehe 17 Januari na kuhitimishwa tarehe 20 Januari 2017.

Kardinali Parolin anasema, katika kipindi cha maisha na uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, shughuli za kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa zinazofanywa na Vatican zimeongezeka maradufu, hasa katika kupambana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa nyakati hizi. Viongozi wakuu wa nchi na Mashirika ya Kimataifa wamekuwa wakikutana mara kwa mara na Baba Mtakatifu Francisko na wengi wao wanamshukuru kwa Waraka wake wa Kitume, juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ulioisaidia pia Jumuiya ya Kimataifa hata kufikia Itifaki ya makubaliano juu ya mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya nchi iliyotiwa sahihi mwaka 2015 huko Paris, Ufaransa.

Baba Mtakatifu katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje anakazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Hapa jambo la msingi anasema Kardinali Parolin ni ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la tatu la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu!

Kardinali Parolin anasema, kwa sasa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya unakabiliwa na changamoto kubwa ya mpasuko wa kisiasa, licha ya mchango wake mkubwa katika ustawi na maendeleo ya watu ndani na nje ya Bara la Ulaya. Hapa kwa mara nyingine tena mkazo unapaswa kuwa ni binadamu na mahitaji yake msingi na wala si maendeleo ya vitu peke yake. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini ni mambo ya hadhara na kamwe yasigeuzwe kuwa ni mambo ya mtu binafsi, ili kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Lengo ni kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na vitendo vya kigaidi ambavyo vinachafua na kudhalilisha dini na imani za watu. Vitendo vya kigaidi anasema Baba Mtakatifu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto ya Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kuvaliwa njuga na kuchukuliwa katika mwelekeo chanya zaidi, badala ya wakimbizi na wahamiaji kuonekana kuwa ni kero na chanzo cha vurugu na vitendo vya kigaidi. Wakimbizi na wahamiaji ni rasilimali na nguvu kazi inayopaswa kutumiwa vyema kwa kuibua sera na mikakati bora kwa wakimbizi na wahamiaji

Kardinali Pietro Parolin anahitimisha hotuba yake kwa kusema, amani ni tunda la haki, ukweli, upendo na uhuru. Ikiwa kama kweli, Jumuiya ya Kimataifa inataka amani ya kudumu, kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kuteta haki msingi za binadamu. Uwajibikaji wa kimaadili unahitajika ili kukomesha tabia ya kutengeneza, kutumia na kulimbikiza silaha za kinyuklia. Amani ya kweli kamwe haiwezi kujengwa katika msingi wa woga na wasi wasi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.