2017-01-20 14:42:00

Agano Jipya na la milele!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 20 Januari 2017 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushinda kishawishi cha ubinafsi na tabia ya waalimu wa sheria wa kutaka kuhukumu. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anatengeneza Agano Jipya na la milele linalopyaisha akili na nyoyo za watu kutoka katika undani wao na wala si katika mambo yanayoonekana kwa nje tu!

Baba Mtakatifu alikita mahubiri yake kwenye Waraka kwa Waebrania 8: 6-13 unaonesha utabiri wa kubadilisha Agano na kupatiwa ahadi bora zaidi; ahadi inayopata utumilifu wake kwa njia ya Kristo Yesu anayewapatia waja wake sheria inayoleta mabadiliko kutoka katika undani wa maisha ya mwamini. Katika Agano Jipya na la milele kuna mabadiliko ya mwelekeo wa maisha, kiasi kwamba, kunakuwepo na usikivu na namna mpya ya kufikiri na kutenda. Kimsingi huu  ni mwelekeo mpya wa kuangalia mambo katika maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Agano Jipya linawapatia nafasi waamini kuweza kubadili nyoyo zao, ili kuweza kuona Sheria na Amri za Mungu kwa mwanga na akili mpya zaidi. Walimu wa sheria walifahamu sheria, lakini kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwahukumu watu, kiasi hata cha kumhukumu Yesu Kristo mateso na kifo cha aibu Msalabani. Ka kufanya hivi, walidhani kwamba, wanatekeleza Sheria na Amri za Mungu katika maisha na utume wao!

Lakini kwa bahati mbaya, mwelekeo wao wa maisha ulikuwa mbali sana na Mwenyezi Mungu; ni watu waliomezwa sana na ubinafsi kiasi cha kujitafuta na kujikweza wenyewe; wakawa ni watu wa kulaani tu. Agano Jipya linalofungwa kwa Damu Azizi ya Kristo Msalabani ni chachu ya mabadiliko kiroho na kiakili. Kristo Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, yuko tayari kusamehe na kusahau kwa wale wote wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Mwenyezi Mungu kamwe haweki kumbu kumbu ya dhambi za binadamu, kwani anasamehe na kusahu kwa sababu anasemehe kweli kweli anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Hapa mwaliko kwa waamini ni kujibidisha kutotenda dhambi na daima kujitahidi kukimbia nafasi za dhambi, ili kutembea katika neema na  mwanga wa huruma na upendo wa Mungu. Waamini wanaposamehewa dhambi zao, wanapaswa kubadilika na kuwa ni watu wapya na wema zaidi, huu ndio uumbaji mpya unaoletwa kwa njia ya Agano Jipya na la milele. Watu wanapaswa kubadilika mintarafu utambulisho wao kwa kutambua kwamba, sasa ni watu wa Mungu ambaye wanapaswa kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao na kuachana na miungu mingine yote.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awajalie neema ya kuwa waaminifu katika Agano Jipya  kwa kubadilika kutoka katika undani wa nyoyo na akili zao kwani Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kubadili moyo wa jiwe kuwa kweli ni moyo wa nyama kama walivyotabiri Manabii kwenye Agano la Kale! Yaani kuwa tayari kuacha kutenda dhambi, ili kutomletea Mungu kichefuchefu cha kutaka kukumbuka dhambi za walimwengu kwani hii si tabia yake. Waamini wasikubali kumezwa na malimwengu, bali wawe tayari kumwambata na kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.