2017-01-19 15:27:00

Waamini simameni kidete kutetea Injili ya uhai na kushuhudia huruma!


Waamini wanaalikwa na kuhamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia inayosimikwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, nchini Ufilippini wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Nne la Huruma ya Mungu Duniani, lililozinduliwa hapo tarehe 16 Januari na linahitimishwa rasmi tarehe 20 Januari 2017 huko Manila, nchini Ufilippini.

Katika maadhimisho ya Kongamano hili, wajumbe wamebahatika kufanya hija ya maisha ya kiroho katika maeneo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ufilippini, ili kujionea wenyewe jinsi ambavyo Familia ya Mungu nchini Ufilippini inavyojitahidi kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha. Haya ni matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanayotekelezwa na Familia ya Mungu nchini Ufilippini kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wagonjwa na wazee; pamoja na huduma kwa waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Lengo ni kuwaonjesha wote hawa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili kwa njia ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu waweze kuwa tayari kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, changamoto ambayo inatolewa pia kwa waamini wote! Waamini wajifunze kutoka katika shule ya Bikira Maria, aliyekuwa na jicho la kimama kwa kuangalia na kuguswa na mahangaiko ya jirani zake, tangu siku ile aliposikia kwamba, binamu yake Elizabeth alikuwa ni mjamzito akaenda kwa haraka. Bikira Maria aliguswa na mahangiko ya wanandoa kule kwenye harusi ya Kana, wakabahatika kupewa divai ya furaha, imani, matumaini na mapendo kutoka kwa Kristo Yesu.

Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu pasi na kificho, kwani waamini wanapaswa kukiri imani kwa midomo yao na kuishuhudia kwa maisha yao yenye mvuto na mashiko! Waamini wanaalikwa kukuza na kudumisha Ibada ya huruma ya Mungu, kiini cha imani inayomwilishwa katika matendo, sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu.

Askofu Ruperto C. Santos wa Jimbo Katoliki Balanga anasema hii ni changamoto kubwa nchini Ufilippini ambayo kwa sasa imetumbukia katika utamaduni wa kifo dhidi ya wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya! Hadi sasa, kuna idadi kubwa ya watu ambao wameuwawa na Serikali kutokana na makosa ya biashara haramu na matumizi haramu ya dawa za kulevya, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa cha Injili ya uhai na haki msingi za binadamu. Anakumbusha kwamba, binadamu anayo dhamana ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko kwani mazingira na uhai wa binadamu ni chanda na pete, au ni “sawa na uji na mgonjwa”. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kujenga utamaduni wa kukuza, kudumisha na kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo laini pamoja na adhabu ya kifo, ambayo kimsingi imepitwa na wakati!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya anawakilishwa na Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lione, nchini Ufaransa. Kongamano la Huruma ya Mungu Duniani hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kuwashirikisha viongozi wa Kanisa na Wasomi na waamini walei kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni fursa ya kufanya hija ya huruma ya Mungu katika maisha ya waamini, tayari kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu ambayo ni chemchemi ya furaha ya kweli, amani na utulivu wa ndani!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha utume wa Kanisa kwa ajili ya wafungwa magerezani, ili kweli haki iweze kutendeka sanjari na kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya wafungwa magerezani vinaheshimiwa na kuthaminiwa, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Magereza kamwe yasiwe ni mahali ambapo utu na heshima ya binadamu havipewi kipaumbele cha pekee!

Askofu msaidizi Broderick Pabillo wa Jimbo kuu la Manila anasema,  Kanisa nchini Ufilippini litaendelea kuhimiza utawala bora unaofumbatwa katika sheria, kanuni maadili na utu wema. Maaskofu wataendelea kukemea utamaduni wa kifo dhidi ya wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya, mintarafu haki msingi za binadamu! Kanisa linasikitika kusema, zaidi ya watu elfu sita tayari wamekwisha uwawa kikatili na Serikali kutokana na tuhuma na makosa ya kujihusisha na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Wengi wao ni maskini ambao hawakutendewa haki wakati wa mchakato mzima wa kesi zao! Kanisa linawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu! Historia ya Ufilippini kwa miaka iliyopita, iwe ni fundisho kwa Serikali iliyoko madarakani, ili makosa yaliyotendwa huko nyuma, yasijirudie tena kiasi cha kuleta madhara tena katika maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.