2017-01-17 10:38:00

Kardinali Agustoni amepumzika katika amani ya Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 17 Januari 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameongoza Ibada ya Maziko ya Kardinali Gilberto Agustoni aliyehitimisha hija ya maisha yake hapa duniani akiwa na umri wa miaka 94. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kumwombea amani na mwanga wa Kristo Mfufuka!

Katika mahubiri yake, Kardinali Sodano amesema kwamba, Makaburi ya Wakristo wengi wa Kanisa la Mwanzo yaliandikwa “Katika Amani ya Kristo”, kielelezo cha imani ya Wakristo hawa katika Fumbo la Ufufuko. Hii ndiyo sala ambayo Kanisa linamwombea Marehemu Kardinali Gilberto Agustoni wakati wa maziko yake, kama sehemu pia ya utekelezaji wa matendo ya huruma kiroho; kumbu kumbu endelevu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliohitimishwa hivi karibuni.

Mama Kanisa anafundisha na kuamini katika Fumbo la Ufufuko wa wafu, ndiyo maana anawahimiza Wakristo kuwahifadhi waamini marehemu kwa heshima, kwani, Kanisa linatambua kwamba, Yesu aliteswa, akafa na kufufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Hii ndiyo njia ya Kristo na wafuasi wake. Liturujia ya Neno la Mungu imewakumbusha waamini dhana ya Fumbo la Kifo linalomwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, lakini akiwa na tumaini la ufufuko kama ilivyokuwa kwa Ayubu aliyekiri kwamba, anajua kwa hakika kwamba, mtetezi wake yu hai na jicho lake litapata fursa ya kumtafakari.

Mwinjili Luka anawahamasisha waamini kuwa daima macho, kwa kukesha na kusali, huku taa zao zikiwa zinawaka, tayari kumpokea Kristo Yesu anapowaita kwenda nyumba kwa Baba yake wa mbinguni. Hii ndiyo imani ambayo imekuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya Kardinali Gilberto Agustoni. Yesu ni nuru ya ulimwengu na kila anayemwamini hawezi kukaa gizani kwani Kristo Yesu ni mwanga angavu uliomwongoza Kardinali Agustoni katika maisha yake hapa duniani. Wengi wao wanamfahamu Marehemu Kardinali Gilberto Agustoni ambaye tangu mwaka 1950 alisadaka maisha yake kwa ajili ya kutekeleza utume wake mjini Vatican, akaendelea kuweka kumbu kumbu ya Jumuiya yake kutoka Uswiss na kwamba, daima alisaidia mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo. Lakini kwa sasa wanamwombea ili aweze kupumzika katika amani ya Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.