2017-01-16 10:09:00

Yohane Mbatizaji alikuwa ni shuhuda wa Kristo Yesu!


Yohane Mbatizaji wakati alipokuwa anawabatiza watu ubatizo wa toba, alimwona Yesu akimwijia akamtambulisha kwa watu kuwa ni Mwana kondoo wa Mungu anayezichukua dhambi za ulimwengu. Wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyojikita kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo.

Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao, kumbe, walitakiwa kutubu na kumwongokea Mungu na kuanza kutembea katika maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa.

Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu anamshukia Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Yesu Kristo ni Masiha wa Bwana. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 15 Januari 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, tukio hili lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji, kumwona Yesu akiwa kati kati ya kundi kubwa la wadhambi kama wao, lakini kwa ajili yao, ili aweze kubatizwa na kutekeleza haki yote sanjari na mpango wa wokovu wa Mungu. Yesu Kristo anajionesha kama Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu.

Yohane Mbatizaji anamtambulisha kwa Yesu kuwa ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Yesu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tafakari ya Neno la Mungu imekita mizizi yake katika tukio hili lisilo la kawaida kwani ni kiini cha imani na utume wa Kanisa linalohamasishwa nyakati zote kumtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwana Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu! Ni Bwana na Mkombozi pekee wa ulimwengu aliyejivika taji la fadhila ya unyenyekevu akathubutu hata kusimama kati kati ya wadhambi, ili kuwakomboa na kuwapeleka kwenye uhuru kamili. Bikira Maria anasema Baba Mtakatifu Francisko ni Mama wa Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu, awasaidie waamini kumwamini na kumfuasa Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.