2017-01-16 10:28:00

Watoto wakimbizi na wahamiaji wahakikishiwe ulinzi na usalama


Mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 15 Januari 2017, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha waamini na mahujaji waliofurika kwa wingi kwenye tukio hili kwamba, Kanisa lilikuwa linaadhimisha Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani. Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa 2017 ni “Wahamiaji wadogo ni wahanga pasi na sauti”. Watoto hasa wale ambao hawasindikizani na wazazi pamoja na walezi wao daima wako hatarini.

Watoto hawa ni wengi sana, kumbe, kuna haja ya kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuwahakikishia watoto wahamiaji na wakimbizi ulinzi, usalama na hatimaye, kuingizwa katika jamii husika. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwasalimia wawakilishi wa wakimbizi na wahamiaji waliofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuungana na Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Siku ya wakimbizi na wahamiaji duniani kwa Mwaka 2017.

Baba Mtakatifu anawataka wahakimbizi na wahamiaji kuishi kwa amani, usalama na utulivu katika maeneo wanayopatiwa hifadhi, kwa kuendelea kulinda, kutunza na kushuhudia tunu msingi za maisha na tamaduni zao asilia kwani mwingiliano wa tamaduni mbali mbali ni kielelezo cha utajiri mkubwa. Amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Shirika la Wakimbizi Jimbo kuu la Roma “Migrantes” pamoja na wale wote wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji.

Papa Francisko amewataka kuendelea kutekeleza dhamana hii kwa kuiga mfano wa Mtakatifu Francesca Saverio Cabrini, msimamizi wa wakimbizi na wahamiaji, ambaye anakumbukwa na Kanisa kwa kutimiza miaka 100 tangu alipofariki dunia. Ni mtawa jasiri aliyejipambanua katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, ili kuwashirikisha na kuwaonjesha huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ushuhuda wake makini, unawahamasisha waamini kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao wakimbizi na wahamiaji, ambao Kristo Yesu kwa njia yao anajitambulisha kati ya watu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema kwa uchungu mkubwa kwamba, hawa ni watu wanaoteseka, wanaobaguliwa na kunyanyasika. Maandiko Matakatifu yanawataka waamini na watu wenye mapenzi mema kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji kwa kukumbuka kwamba, hata wao ni wakimbizi na wahamiaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.