2017-01-16 10:45:00

Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 15 Januari 2017 ametembelea Parokia ya Santa Maria Setteville di Guidonia Jimbo kuu la Roma na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu, amekutana na makundi mbali mbali ya maisha na utume wa Parokia pamoja na kumtembelea Padre Giuseppe Berardino ambaye amepooza kitandani kwa muda wa miaka miwili sasa. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amewaelezea waamini jinsi ambavyo Yohane alivyomtambulisha Yesu kwa wafuasi wake nao wakaamua kumfuasa Kristo katika maisha yao yote kutokana na furaha waliyokutana nayo kwa kumwona Yesu Kristo.

Yohane ni shuhuda amini wa Kristo Yesu, changamoto kwa familia ya Mungu kwa nyakati hizi, kuendelea kumshuhudia Kristo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo ambayo ni kielelezo amini cha imani tendaji. Mitume wa Yesu walijitaabisha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mitume walibahatika kufundwa na Kristo Yesu kwa muda wa miaka mitatu na baadaye kazi hii iliendelezwa na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema hawa ni watu wa kawaida, wavuvi kutoka Galilaya, walikuwa ni wadhambi lakini huruma na upendo wa Mungu uliweza kuwangoza kiasi hata cha kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake. Yuda Iskarioti ni kati ya wale waliomsaliti Yesu; Mtume Petro akamkana Yesu mara tatu na wengine walikimbia na kutokomea mbali wakati Yesu alipokamatwa, akateswa na kufa Msalabani. Kumbe, shuhuda ni yule mwamini anayetambua kuwa ni mdhambi, lakini anajibidisha kumshuhudia Kristo Yesu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa imani yake yenye mvuto na mashiko. Anapoanguka dhambini kutokana na udhaifu wa kibinadamu, yuko tayari kusimama kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kusonga mbele katika safari ya maisha ya Kikristo!

Baba Mtakatifu anasema, hata miongoni mwa Mitume walikuwemo wenye misimamo mikali, waliotaka kuwashikisha adabu wale watu waliokataa kumpokea Yesu kijijini kwao. Ujumbe makini ambao Baba Mtakatifu amependa kuwaachia waamini wa Parokia ya Santa Maria Setteville di Guidonia Jimbo kuu la Roma ni kujikita katika fadhila ya unyenyekevu, ukweli na uaminifu; umoja, upendo na mshikamano wa kweli, tayari kumtolea Kristo Yesu ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Parokia iliyosheheni umbeya haina mvuto, kama kuna “bifu” basi watu wawe na ujasiri wa kuambiana ukweli, ili kusaidiana na kurekebishana kadiri ya upendo wa Kikristo kwa kutambua kwamba, wote ni wa dhambi na wanahitaji huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo kama walivyofanya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.