2017-01-16 11:58:00

Viongozi jengeni uwajibikaji kwa kuzingatia kanuni maadili!


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, kuna haja ya kuwa na utandawazi wa kanuni maadili ili kuweza kukabiliana kinagaubaga na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na vitendo vya kigaidi ambalo linaonekana kuwa ni janga kubwa linalohatarisha maisha na mafungamano ya kijamii duniani; athari za mabadiliko ya tabianchini; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, nyanyaso na ubaguzi wa kila aina.

Dhana ya uwajibikaji wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa mintarafu kanuni maadili ni muhimu sana ili kuweza kufikia muafaka wa kuweza kukabiliana na changamoto hizi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Dr. Tveit ameyasema haya wakati viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanakutana mjini Davos, Uswiss kuanzia tarehe 17- 20 Januari 2017 ili kushiriki katika Jukwaa la Uchumi Duniani. Kati ya tema zinazojadiliwa ni imani, utu na heshima ya binadamu; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; vitendo vya kigaidi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi katika mchakato wa kukuza na kudumisha uchumi na maendeleo ya wengi.

Ikiwa kama viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawatawajibika barabara kwa kujikita katika kanuni maadili, ustawi na mafao ya wengi, mchakato wa utandawazi na maendeleo ya watu, yataendelea kuchechemea na athari zake kuwa ni kubwa kila kukicha! Uwajibaki wa pamoja na hali ya kuaminiana ni muhimu katika utekelezaji wa maamuzi yanayofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Mwaka 2017 uweni ni fursa kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kumbu kumbu.

Dr. Tveit anasema, Mwaka 2017 ni mwaka wa neema na matumaini ya ajabu kwani Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wataadhimisha Siku kuu ya Pasaka na Pentekoste siku moja, fursa ya kuwaunganisha watu wa Mungu walioko Nchi Takatifu ili kusali kwa ajili ya kuombea amani, upendo na mshikamano wa dhati. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kufanya maandalizi ya kina, ili kuweza pia kuwashirikisha wajumbe kutoka katika Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala, maisha ya kiroho, damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Dr. Tveit anasema, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya Makanisa mbali mbali na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuimarisha mchakato huu ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Anasema, mezani kwake anazo barua mbili kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ya kwanza ni salam na matashi mema kwa Siku kuu ya Noeli na pili ni Barua ya Mwaliko kwa ajili ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017. Wakristo wanapaswa kuungana pamoja, ili kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kama sehemu ya mchango wake katika huduma kwa walimwengu.

Katika mwelekeo huu, vijana wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanasismama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya amani, upatanisho na maridhiano duniani. Mjini Davos, kuna kundi la vijana waliozaliwa kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 2000, hawa wanajulikana kama “millenials”! Hili ni kundi la vijana ambalo lina ufahamu mpana zaidi kuhusu tunu msingi za kijamii, utu wa binadamu na umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani. Umefika wakati wa kutoa nafasi kwa vijana ili kuweza kushirikisha karama na vipaji vyao kwa ajili ya ujenzi wa dunia ili bora zaidi pamoja na kuondokana na mtindo wa sasa wa kuwatupia vijana “madongo” kila wakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.