2017-01-16 13:18:00

Prof. Alpha Condè akutana na kuzungumza na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Januari 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Alpha Condè wa Jamhuri ya Guinea ambaye baadaye amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu na Professa Condè katika mazungumzo yao ya faragha wamesifia uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Guinea. Baadaye, wamejielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki jamii pamoja na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Katika mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo, viongozi hawa wawili wameridhika na mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini Guinea katika ustawi na maendeleo ya wengi hususan katika sekta ya elimu, afya pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Waislam na Wakristo nchini humo. Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake wamejielekeza katika masuala ya Kikanda hasa zaidi mchango wa Guinea katika ujenzi wa amani na mshikamano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.