2017-01-14 15:45:00

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais Mahmoud Abbas


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 14 Januari 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Mohmoud Abbas wa Mamlaka ya  Wapalestina ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekua ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, katika mazungumzo yao, wamefurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Palestina ulioimarishwa kwa pande hizi mbili kutiliana sahihi Itifaki ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Mwaka 2015 unaojikita zaidi katika maisha na utume wa Kanisa katika Jamii ya Wapalestina. Wamefurahishwa pia na mchango unaotolewa na Kanisa katika huduma za kibinadamu hasa zaidi katika sekta ya elimu, afya na huduma za kijamii.

Baadaye, viongozi hawa wawili wamejikita zaidi katika mgogoro wa kivita unaoendelea kufuka moshi huko Mashariki ya Kati, hali ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, changamoto ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya haki na ya kudumu. Viongozi hawa wanatumaini kwamba, kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa, hatua madhubuti zinaweza kuchukuliwa ili kusaidia pande zinazohusika kujenga hali ya kuaminiana itakayosaidia wadau kuweza kutoa maamuzi mazito kwa ajili ya kujenga na kudumisha amani. Viongozi hawa wamekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha utakatifu wa Maeneo Matakatifu ambamo waamini wa dini kuu tatu wanayaheshimu na kuyatukuza. Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko na Rais Mohmoud Abbas wa Palestina wamegusia pia maeneo mengine yenye vita, kinzani na migogoro ya kijamii katika Ukanda huo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.