2017-01-14 15:57:00

Marehemu Kardinali Gilberto Agustoni kuzikwa tarehe 17 Januari 2017


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Gilberto Agustoni kilichotokea tarehe 13 Januari 2017. Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Mama Luisa Santandrea, mpwa wake Marehemu Kardinali Agustoni anapenda kumtumia salam zake za rambi rambi kwake binafsi, ndugu na jamaa pamoja na wote walioguswa na msiba huu mzito. Kwa miaka mingi Marehemu Kardinanli Agustoni alikuwa ni mshauri wa karibu sana wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Kanisa Katoliki, akajitahidi kutoa ushuhuda wa ari, moyo, huduma pamoja na uaminifu kwa Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu anaiombea roho ya Marehemu Kardinali Agustoni kwa Kristo Yesu, ili kwa maombezi ya Bikira Maria, akipenda aweze kumpatia tuzo ya maisha ya uzima wa milele Kardinali Agustoni kama alivyowaahidia waja wake. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kutoa baraka zake za kitume kwa wote walioguswa na msiba huu mzito.

Taarifa za mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa Monsinyo Guido Marini inaonesha kwamba, Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, tarehe 17 Januari 2017, majira ya saa 4:00 kwa saa za Ulaya ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye, Baba Mtakatifu Francisko atahitimisha kwa Ibada ya Maziko kwa Kardinali Gilberto Agustoni.

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Agustoni alizaliwa kunako tarehe 26 Julai 1922 Jimboni Basel, nchini Uswiss. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 20 Aprili 1946 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 18 Desemba 1986 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na kumweka wakfu tarehe 6 Januari 1987. Tarehe 26 Novemba 1994 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Kardinali. Baada ya huduma makini kwa Kanisa la Kristo, tarehe 13 Januari 2017 akiwa mjini Roma, akaitwa kwenda kwenye makao ya milele!

Katika maisha na utume wake ni kiongozi wa Kanisa aliyebahatika kuonesha karama na mapaji mbali mbali kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo. Alibahatika kuwa ni kiongozi makini kwa utume wa vijana! Alipewa dhamana na majukumu mbali mbali mjini Vatican katika Mahakama kuu ya Kanisa Katoliki; Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, akaandaa kwa weledi mkubwa, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya majiundo awali na endelevu kwa Wakleri. Alikuwa ni mjumbe wa Kamati ya Kuhariri Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Katiba ya Kitume ya ”Pastores dabo vobis” inayoratibu shughuli mbali mbali zinazofanywa na Sekretarieti kuu ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.