2017-01-14 14:34:00

Kilele cha Mwaka Padre Tanzania: 15 Agosti 2017 Jimboni Dodoma


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mapadre kwa ajili ya Daraja Takatifu na ya utume wanayopewa na Maaskofu, wanapokelewa kumtumikia Kristo aliye, Mwalimu, Kuhani na Mfalme; nao wanashiriki huduma yake ambayo kwayo hapa duniani Kanisa hujengwa bila kukoma kuwa Taifa la Mungu, Mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Mapadre kimsingi ni wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Mapadre ni walezi wa Taifa la Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anaongeza kwa kusema, wito na maisha ya Upadre ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ameweka moyoni mwa baadhi ya waamini, kumbe ni wajibu na dhamana ya Kanisa kuhakikisha kwamba, wale wote wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake wanapata malezi makini na endelevu katika maisha, wito na utume wa Kipadre, ili waweze kuzaa matunda ya ukomavu na utakatifu wa maisha na hatimaye waweze kung’aa kati ya watu wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Mwaka 2017 linaadhimisha Mwaka wa Padre, kama kumbu kumbu endelevu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Mapadre wakwanza wazalendo walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre kunako Mwaka 1917. Sanjari na maadhimisho haya, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendelea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara na kilele chake ni hapo Mwaka 2018. Kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Padre kitakuwa Jimbo kuu la Dodoma, tarehe 15 Agosti 2017, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Kupalizwa Bikira Maria mbinguni!

Haya yamebainishwa hivi karibuni na Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida wakati alipokuwa anatoa Daraja ya Ushemasi wa Mpito kwa Majandokasisi wawili wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu; Ibada iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Damu Azizi ya Yesu, Itigi, Jimbo Katoliki Singida. Majandokasisi waliopewa Ushemasi wa mpito ni Dominic Mavulla na Alessandro Manzi. Maadhimisho ya kilele cha Mwaka wa Padre, Jimbo kuu la Dodoma ni heshima kubwa ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania imetoa kwa Jimbo kuu la Dodoma linaloundwa na Majimbo ya Singida na Kondoa. Familia ya Mungu katika Majimbo haya inayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa upendeleo huu.

Askofu Mapunda anaendelea kutoa mwito kwa waamini kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ili kweli Kanisa la Mungu nchini Tanzania liweze kupata watendakazi wema, watakatifu na wachapakazi. Mwaka wa Padre Tanzania unakwenda sanjari na maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana itakayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Hiki ni kipindi cha kufanya tathmini ya kina kuhusu sera na mikakati ya majiundo awali na endelevu kwa ajili ya Mapadre ili waweze kung’ara kama nyota angavu kati ya Watu wa Mungu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa.

Askofu Mapunda katika mahubiri yake amewakumbusha waamini kwamba, Jubilei ni ni muda wa kushukuru, kutubu, kuomba na kujiwekea mikakati ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, tayari kutekeleza maongozi ya Mungu katika maisha. Wamissionari wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kitume wamekuwa ni chachu na mbegu ya miito ya kipadre na kitawa, Kanisa la Tanzania linapaswa kuonesha moyo wa shukrani kwa kuendelea kukuza na kudukisha miito ya Kipadre na Kitawa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Waamini katika safari ya maisha yao, wajenge tabia na utamaduni wa kufanya hija, kumtafuta na hatimaye, kumwambata Mungu katika maisha yao.

Askofu Edward Mapunda amewataka Wakleri kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu ili kuzima kiu na njaa ya maisha ya kiroho kwa waamini wao. Wakleri wawe wepesi kwenda kusikiliza kilio cha damu na kujifunza mahangaiko ya watu, tayari kuyapatia majibu muafaka yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake kama alivyofanya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, leo hii Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu linasonga mbele kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu ndani nan je ya Tanzania.

Siku iliyotangulia Ushemasi, Padre Chesco Peter Msaga aliongoza Ibada ya kumpokea rasmi Shirikani, Frater Domini Mavulla kwa kumtaka awe ni shuhuda wa mwanga unaong’ara ili kufukuza giza katika maisha ya watu wa Mungu. Mihimili ya Injili inapaswa kujisadaka zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama kielelezo cha imani tendaji! Ni mwaliko wa kuendelea kuwagawi waamini Mafumbo ya Kanisa ili waweze kutembea katika mwanga, neema na utakatifu wa maisha, tayari kumwabudu Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kuendelea kutangaza Mwaka wa Bwana uliokubalika kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa Maadhimisho ya Jubilei  ya huruma ya Mungu, ili kweli watu waguswe na huruma pamoja na upendo wa Mungu katika safari ya maisha yao ya kila siku! Hii ndiyo Dira na Mwongozo wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu katika kipindi cha miaka kumi!

Na Rodrick Minja kutoka Dodoma na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.